Tamasha la filamu za Beijing Afrika lazinduliwa Dar

Msimu wa Matangazo ya Tamthiliya na Filamu za Televisheni za Beijing Afrika umefunguliwa rasmi Dar es Salaam, ukiongozwa na Idara ya Televisheni na Redio ya Beijing.

Tamasha hilo linaadhimisha miaka 10 ya ushirikiano thabiti kati ya Beijing na nchi za Afrika kupitia maonyesho ya filamu bora, likiimarisha urafiki na mawasiliano ya kiutamaduni kati ya China na Afrika.

Sherehe za uzinduzi zimefanyika Dar es Salaam na kuhudhuriwana viongozi kutoka Idara ya Televisheni na Redio ya Beijing, Bodi ya Uendelezaji wa Filamu ya Tanzania, Baraza la Sanaa la Tanzania (Basata) na wadau mbalimbali wa sekta ya filamu kutoka pande zote mbili.

Advertisement

Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Televisheni na Redio ya Beijing, Dong Dianyi, amesema kuwa tamasha hili limekuwa daraja muhimu la mawasiliano ya kiutamaduni kati ya China na Afrika.

“Miaka kumi iliyopita, tamasha hili lilianza barani Afrika, na sasa limekuwa alama ya urafiki wa kweli kati ya watu wa pande hizi mbili. Tunatazamia kuendelea kuimarisha ushirikiano huu katika miaka ijayo,” amesema.

Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Bodi ya Filamu ya Tanzania, Emmanuel Ndumukwa, amesema kuwa tamasha hilo limechangia kwa kiasi kikubwa katika ukuzaji wa sekta ya filamu nchini Tanzania.

Ametoka mfano wa mafanikio ya filamu kama Karibu Kijijini Milele, ambayo ilitafsiriwa kwa Kiswahili na lugha nyingine, na hata kushinda “Tuzo maalum ya kuchangia urafiki kati ya China na Tanzania.

”Tamasha limeleta filamu mpya zenye maudhui mbalimbali, ikiwemo karibu kijijini Milele, inayosimulia safari ya ushirikiano kati ya China na Afrika, na Shuke na Beta, filamu ya katuni itakayovutia watoto wa Afrika. Kwa njia hii, tamasha linahakikisha linakidhi ladha za watazamaji wa rika zote,”amesema.

Amesema kwa mara ya kwanza, tamasha limepanua jukwaa lake hadi mtandaoni kupitia programu ya Scooper, ambapo pembe mbalimbali za utamaduni wa Kichina zinawasilishwa kwa watazamaji wa Afrika.

Ndumukwa amesema tangu 2014, tamasha hili limewafikia watu katika nchi 13 za Afrika, zikiwemo Kenya, Nigeria, na Afrika Kusini, likionesha filamu 148 kwa lugha kama Kiswahili, Kiingereza, na Kifaransa. Mbali na maonyesho ya filamu, tamasha limeleta matukio kama mashindano ya upigaji sauti wa filamu, maonyesho ya sanaa ya mapigano, na shughuli za katuni kwa watoto, likieneza utamaduni wa China kwa njia ya kuvutia na shirikishi.

Mwisho