Tamasha la Msangamkuu Beach lazinduliwa

MKUU wa Wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya amezidua rasmi Tamasha la Msangamkuu Beach Festival msimu wa nne linalofanyika katika Kata ya Msangamkuu Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, mkuu huyo wa wilaya amesema tamasha hilo linatoa fursa ya kuhamashisha utalii mbalimbali uliyopo mkoani humo ikiwemo fukwe za bahari, kuonyesha fursa za uwekezaji katika seketa ya utalii.
Fursa nyingine ikiwa ni pamoja na kuchangia katika kuhamasisha utalii wa ndani na kusisitiza kuwa utalii haupaswi kuhusishwa na wageni pekee bali hata wananchi waliyopo ndani ya mkoa huo wanapaswa kushiriki kikamilifu kwenye tukio hilo.

Aidha tamasha hilo licha kutoa fursa katika sekta ya utalii lakini linahusisha michezo mbalimbali ikiwemo ya ufukweni, mpira wa miguu, mashindano ya kuogelea, masumbwi pamoja na burudani kutoka kwa wasanii ndani na nje ya mkoa huo.
‘’Mkoa wetu umebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya kitalii lakini pamoja na vivutio hivyo ukuaji wa sekta ya utalii ni mdogo sana kwahiyo tamasha hili ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya kuhakikisha sekta hii inaongeza mchango katika uchumi wa wananchi wa mkoa wetu wa mtwara na taifa kwa ujumla,’’amesema Mwaipaya.
Amevitaja baadhi ya vivutio vya kitalii vilivyopo mkoani humo ikweimo mji mkongwe wa mikindani uliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, uwepo wa nyangumi kwenye fukwe za bahari, shimo la Mungu lililopo wilayani Newala.
Hata hviyo mila na desturi za makabila ya wamakonde na wamakuwa, ziwa Chidya lililopo katika kijiji cha kitaya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara na vingine.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Nanjiva Nzunda amesema tamasha hilo licha ya kutangaza vivutio hivyo vya kitalii lakini linaleta upendo na faraja baina yao na linaondoa mawazo hivyo wana kila sababu ya kuhakikisha wanapambana na hali hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Msangamkuu Beach Festival, Athuman Kambi amesema malengo ya kamati hiyo ni kuhakikisha kuwa, katika miaka ijayo tamasha hilo linaratibiwa na wafanyabiashara pamoja na wajasiliamali ili kupunguza mzigo wa kiutawala wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
Aidha, tamama la Msangamkuu Beach Festival mwaka 2024 linatarajiwa kupambwa na burudani kutoka kwa msanii maarufu nchini wa Bongo Fleva Harmonize pamoja na wasanii wengine kutoka mkoani mtwara.



