KAMPUNI ya Azam Media imetambulisha tamthilia za Kitanzania tatu zinazofahamika kama Tufani, Kiki pamoja na Kombolela msimu wa pili.
Tamthilia hizo zenye visa na mikasa zimebeba simulizi na kuleta mapinduzi makubwa katika tasnia ya tamthilia, kutoka kampuni tatu tofauti za wasanii mbalimbali ikiwa ni mwendelezo wa kuwaunga mkono wasanii kupitia kazi wanazofanya kuburudisha na kuelimisha jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari Katika uzinduzi wa tamthilia hizo jijini Dar es Salaam leo, Msimamizi Mkuu wa Sinema Zetu Sophia Mgaza amezitaja tamthilia hizo kuwa ni Tufani iliyoandaliwa na kampuni ya Jacob Steven ‘JB’, Kombolela iliyoandaliwa na Nabra Creative na Kiki iliyoandaliwa na Magazijuto Company chini ya Mtiti.
Sophia amesema tamthilia hizo zimesheheni mastaa mbalimbali wakiwemo Jacob Steven’JB’, Abdul Juma, William Mtitu, Mariam Ismail Julieth Samson ‘Kemmy’ , Albert Mlilo, Kulwa Kikumba ‘Dude’,Shamira Ndwangila ‘Bi Star ‘na wengine wengi.
“Sinema Zetu inawasogezea burudani sebuleni kwako wakongwe wa uzalishaji wa filamu na tamthilia nchini kwa pamoja wakiwa ndani ya tamthilia tatu kali za kipekee zilizosheheni waigizaji nguli wabobevu wa Sanaa, wasomi wa vyuo vikuu pamoja na wasanii wanaochipukia, yote hiyo ni kuwaunga mkono wasanii wetu wainuke kiuchumi,”alisema.
Amesema tamthilia ya Tufani inaangazia familia mbili ya Mrs Komba (Single parent’s) na mwenye watoto watatu anayejikita katika biashara ngumu zinazodhalilisha utu wake ili mtoto wake mkubwa asome vizuri.
“Ili baadaye aje kuwasaidia wadogo zake wawili mara baada ya kusoma na kupata ajira lakini anazima ndoto za mama yake baada yakuangukia penzi la msichana kahaba anayeuawa hotelini na mwisho wa siku anamfunga mama yake jela.”
“Kuhusu tamthilia ya Kombolela amesema ni ya kifamilia yenye misuguano na migogoro na masimango inayoonesha maisha halisi ya Watanzania wa tabaka la chini wanayoishi katika harakati zao za kujenga familia na kujitafutia kipato.”amesema
Kwa upande wa Tamthilia ya Kiki inaelezea maisha ya mfanyabiashara maarufu kigogo aliyeamua kujikita kwenye mbio za urais ili kulinda biashara yake nayo ikiwa imesheni visa mbalimbali lakini ikiwa na elimu ndani yake.
Amesema tamthilia ya Tufani itaanza kuoneshwa kuanzia Disemba 9, mwaka huu, itaruka kuanzia Jumatatu hadi Alhamis na Kombolela kuanzia Disemba 13 Ijumaa hadi Jumapili huku Tamthilia ya Kiki kuanzia Disemba 16 Jumatatu hadi Alhamis kwenye Chanel ya Sinema Zetu.
“Lengo la Azam Media ni kuendelea kutoa burudani ya hali ya juu kwa watazamaji wetu huku tukisukuma Sanaa yetu kimataifa hasa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na popote,”amesema Sophia
Kwa upande wake Jacob Steven ‘JB’ amesema tupo kwenye ushindani na kunaendelea kushindana mashabiki wakae mkao wa kula.