Tanapa yaandaa mtoko siku ya wanawake
KUELEKEA siku ya wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 2, 2024, Mamlaka za Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia(TAZARA) wanaanda mtoko maalum kwa ajili ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kujionea vivutio vilivyopo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Kamishina wa TANAPA , Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini mwa Tanzania ,Steria Ndaga alisema mtoko huo wa siku moja utahusisha usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam hadi hifadhini na kurudi na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali.
Amesema watakaotembelea watapata fursa ya kuingia katika hifadhi na kuona wanayama,ndege,mabwawa mbalimbali na watapata vyakula na vinywaji wakiwa ndani ya hifadhi.
“Lengo ni kuhamasisha wanawake kushiriki katika utalii na uhifadhi na kujua umuhimu wake, hafla itanzia Dar es Salaam na kutembelea Hifadhi ya Taifa Nyerere ili kwenda kuona vivutio mbalimbali vilivyopo na kutoa taarifa za vivutio vya taifa Tanzania na kama TANAPA tunashirikiana wenzetu wa chama cha wanawake wa TAZARA.
Amesema gharama ya mtoko huo kwa mtu mmoja ni Sh 200,000 ambapo itahusisha huduma zote ikiwemo usafiri na chakula.
Aidha katika mtoko huo amesema wanatarajiwa kuwafikia zaidi ya wanawake 400 kutoka maeneno mbalimbali huku wanaume pia wakikaribishwa kushiriki.
“Lengo ni kuona uhifadhi unaendelea na kuhamasisha watanzania kupitia siku ya wanawake kila mmoja aone umuhimu na fursa zilizopo katika hifadhi na wanawake katika umoja wetu tukitumia hizo fursa tutaendeleza jitihada za Rais Samia ambaye amejitoa kuhakikisha uhifadhi unaendelea na kupia filamu ya royal tour tumeongeza wataalii”.amesisitiza.
Amesema watakaohudhuria wanatakiwa kujiandikisha kwa kutembelea kurasa za kijamii za TANAPA watapata taarifa zaidi waweze kulipa.
Kwa upande wake dereva wa treni kutoka TAZARA , Judith Ligenzi amewahamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kuona kazi za wanawake wenzao kwani wengine wanasikia kuna madereva wanawake wanaendesha treni na wengine hawaamini.
“Niwahakikishie tupo na tunajiamini na tutaendesha treni kutoka Dar es Salaam hadi Nyerere nakurudi tukiwa salama na tumeona tutengeneze hii kwasababu reli yetu ya TAZARA inapita mbugani na watu watatumia usafiri wa treni ni kilometa 200 kufika eneo la hifadhi.
Amesema katika mtoko huo kutakuwa na wanawake kutoka makundi mbalimba kama taasisi,mashirika,vyuoni na kuwasisitiza wajitokeze kufurahi pamoja kwa kutumia usafiri wa treni na kutembelea hifadhi.