TANAPA yajivunia miaka mitatu ya Rais Samia

DAR ES SALAAM: SHIRIKA la hifadhi za Taifa TANAPA limesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kuanzia mwezi Julai 2023 hadi Machi 19, 2024 shirika limekusanya Sh bilioni 340, ukilinganisha na matarajio ya kukusanya Sh bilioni 295, mpaka Machi 2024.

Hayo yamesemwa Machi 21, 2024 na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Juma Kuji katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari unaoratibiwa na ofisi ya msajili wa hazina kuelezea mafanikio ya TANAPA kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani.

Amesema kiasi hicho cha Sh bilioni 340 ni ongezeko la Sh bilioni 44, ambayo ni sawa na asilimia 15 huku shirika likiwa na matarajio ya kukusanya kiasi cha Sh bilioni 382, hadi Juni 2024.

Kuhusu ongezeko la watalii nchini na namna ya kuongeza vivutio katika hifadhi za Taifa na kuboresha huduma za watalii Naibu Kamishna uhifadhi, Herman Batio amesema wameendelea na uhamasishaji wa utalii katika ukanda wa Magharibi ikiwemo ujenzi wa hoteli ya kisasa yenye hadhi ya nyota 3 katika hifadhi ya Taifa Chato.

Akizungumzia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha zege ndani ya hifadhi za Taifa kama vile serengeti Kamishna uhifadhi msaidizi TANAPA Dk Richard Matoro amesema changamoto ni upatikanaji wa fedha kwa kuwa gharama ni kubwa kutokana na ukubwa wa maeneo ya hifadhi hizo, na wanachofanya sasa ni kuendelea na maandiko kuona namna gani watatatua changamoto hiyo huku wakiendelea kuzikarabati ili ziweze kupitika.

Mwenyeketi wa jukwaa la wahariri nchini (TEF), Deodatus Balile ameishauri TANAPA kuhakikisha wanalinda sehemu za maziko ya viongozi mbalimbali wa Taifa na kufanya kama sehemu za kumbukumbu za taifa pamoja na kujenga maktaba ya wazi ya meno ya Tembo kuhamasisha watu kuacha uwindaji haramu wa wanyama hao.

Habari Zifananazo

Back to top button