TANESCO waanza utekelezaji maagizo ya Rais Samia

SHIRIKA la Umeme Nchini (TANESCO) limeanza kutekeleza maagizo ya Raisi Dk Samia Suluhu Hassan ya kutaka shirika hilo kuboresha upatikanaji wa umeme kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara.

Sehemu ya maagizo hayo ni kuleta mtambo mkubwa katika mikoa hiyo wa kuzalisha umeme kutumia gesi asilia.

Mkurungezi Mtendaji wa shirika la TANESCO Gissima Nyamo-Hanga leo Januari 11, 2024 ametembelea na kukagua eneo la Hiari Wilaya ya Mtwara ambalo mtambo huo utasimikwa kwa ajili ya kuzalisha umeme huo kitumia gesi asilia.

Amesema mtambo huo ambao utahamishwa kutoka kituo cha kuzalisha umeme cha Ubungo utaletwa mkoani Mtwara ambapo utasaidia kuzalisha umeme kutumia gesi asili kwa ajili ya mikoa ya Lindi na Mtwara.

Nyamo-Hanga amesema ujio wa mtambo huo mkubwa kutoka Ubungo utasaidia kuzalisha megawatts 22 ambazo zitatumika kuimairisha upatikanaji wa umeme

“Tutakuwa na silaha mbili kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la umeme katika mikoa ya Mtwara na Lindi,” amesema.

Kwa sasa mikoa ya Lindi na Mtwara inatumia umeme ambao unazalishwa kutoka kituo ambacho kipo Mtwara Mjini chenye uwezo wa kuzalisha megawatts 21- 22. Mahitaji ya umeme kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara ni megawatts 22.

Katika hatua nyingine, Nyamo-Hanga amesema ujenzi wa kituo cha kusimika mtambo huo mkubwa wa kuzalisha umeme unatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka huu. Amesema maandalizi ya kutoa mtambo na kuusafirisha kuja mkoani Mtwara yameshaanza.

Habari Zifananazo

Back to top button