Uwanja wa ndege Sumbawanga tayari kwa matumizi

SUMBAWANGA: MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imefanya majaribio ya kutua na kuruka kwa ndege katika kiwanja cha ndege cha Sumbawanga baada ya kukamilika kwa ujenzi wake.
Majaribio hayo yamefanyika leo kwa kutumia ndege ya Shirila la Ndege la Tanzania (ATCL) ambayo ilitua katika kiwanja hicho kutoka Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere(JNIA), Dar es Salaam kupitia Kiwanja cha Ndege cha Dodoma.
Akizungumza katika hafla ya majaribio hayo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema majaribio hayo ni hatua ya msingi ya kuthibitisha ubora wa kazi iliyotekelezwa na kupima ubora wa miundombinu kabla ya kuanza kutumika.
“Hatua hii inadhihirisha uwekezaji uliofanyika umezingatia viwango vya kitaifa na kimataifa tayari kutoa huduma salama bora yenye viwango vya miundombinu hii na utayari wa kuanza kufanya kazi na hivyo kuweka msingi imara wa utoaji wa huduma bora na endelevu kwa watumiaji wa usafiri wa anga,” amesema Kihenzile.

Ameeleza kuwa maboresho ya uwanja huo ambayo yamegharimu Sh bilioni 60.1 yanahusisha ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, jengo la abiria lenye uwezo wa kubeba abiria 150,000 kwa mwaka, eneo la kuongoza ndege pamoja na mifumo ya usalama.
Alisema kukamilika kwa miundiombinu hiyo ni hatua muhimu ya kuelekea kwenye kuanza kwa matumizi rasmi ya kiwanja hicho.
Kihenzile amesema kukamilika kwa kiwanja hicho ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya uchumi na kijamii kwa mkoa wa Rukwa na mikoa ya jirani na nchi kwa ujumla.

Amesema kwa kuwa sekta ya uchukuzi ni sekta wezeshi, kiwanja hicho kitawezesha mambo mengi ikiwa ni pamoja na kukuza utalii, biashara, kilimo na sekta zingine kwa kurahisisha usafiri.
Aliagiza ATCL kutoa utaratibu wa siku rasmi ya kuanza safari na kukubali ombi la Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly kwamba kuwepo na safari mbili kwa wiki za Sumbawanga kwa kuanzia na kumwagiza Mkurugenzi wa ATCL, Peter Ulanga kulitekeleza hilo.
“Mamlaka ya Viwanja vya Ndege hakikisha miundombinu yote inatunzwa na kuendeshwa kwa viwango vya kitaifa na kimataifa, muimarishe matengenezo endelevu. Wananchi lindeni miundombinu hii, nyie ndio mnaofaidika, hizi ni kodi zetu wakitekea watu wakavamia miundombinu hii mkawaacha mnatenda makosa kwa vizazi vyenu,” alifafanua Kihenzile.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mapinduzi katika sekta ya anga na kwamba amewezesha mambo mengi yaliyokuwa yamesimama kwa muda mrefu yameanza kufanya kazi kikiwa ni pamoja na kiwanja hicho ambacho kilukuwepo muda mrefu na kilihitaji kukarabatiwa na yeye ndiye aliyefanga maamuzi na kufikia kilipo sasa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mombokaleo alisema Septemba 2023 serikali ilianza kutekeleza mradi huo wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho uliogharimu Sh bilioni 60.1.
“Gharama hizo zilijumuisha ujenzi wa jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 150,000 kwa mwaka, ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami, mifumo ya taa ya kuongozea ndege itakayoruhusu kufanya kazi saa 24, ujenzi wa viungio kwa kiwango cha lami, ujenzi wa maegesho ya ndege kwa kiwango cha lami , ujenzi wa uzio wa usalama , ujenzi wa barabara ya kuingia kiwanjani na ujenzi wa kituo cha hali ya hewa , “ alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Peter Ulanga amesema uwepo wa kiwanja hicho kunafanya shirika kufikia malengo yake ya kusafirisha Watanzania wengi zaidi na kwamba majaribio yaliyofanyika ni mwanzo wa kuanzisha safari zake kuanzia Mei, mwaka huu.



