- MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Maharage Chande amewaomba watanzania kuombea nchi ipate mvua za haraka ili kuvinusuru vituo vya umeme ambavyo mabwawa yake yameanza kupungukiwa na maji ya kuzalisha nishati hiyo kwa viwango vyake.
“Kuna changamoto ya kupungua kwa maji katika mabwawa ya Mtera, Kihansi na Kidatu. Kama mvua za vuli zitachelewa uzalishaji wa umeme utapungua katika mabwawa hayo,” alisema.
Akizungumza mbele ya kamati ya bunge ya Nishati na Madini baada ya kutembelea hali ya uzalishaji wa umeme katika bwawa la Kidatu, Chande alisema kukua kwa uwekezaji kumeongeza pia matumizi ya umeme.
“Vituo vyetu vya kuzalisha umeme vinafanya kazi vizuri, tuombe mvua zinyeshe mapema ili uzalishaji usiathirike, vinginevyo tutapata upungufu,” alisema.
Awali Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga alimshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan akisema dhima yake ya kufikisha umeme kwa watanzania wote inaendelea kudhihirika.
Aliwatoa hofu watanzania na kuwataka kutunza na kulinda vyanzo vya maji alisema vyanzo vya umeme vinajitosheleza na vinafanya kazi kwa ufanisi.
Alisema Juni 2024 Tanzania itakuwa na umeme wa uhakika zaidi kwani bwawa la Mwalimu Nyerere linatarajiwa kuanza uzalishaji wake.
Mbali na Sh Bilioni 20 zilizotolewa kwa ajili ya ukarabati na maboresho ya vituo vya kuzalishia umeme vya Mtera, Kihansi na Kidatu, alisema Dk Samia ametoa pia Sh Bilioni 5 kwa ajili ya kulinda na kuhifadhi mazingira, yakiwemo ya vyanzo vy maji.
“Wito wetu kwa wananchi washirikiane na serikali na wadau wengine kutunza na kulinda vyanzo hivyo ili uzalishaji wa umeme katika vituo hivyo uwe wa uhakika,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ussi Salum Pondeza alihimiza suala la kutunza na kulinda vyanzo vya maji akisema hatua hiyo itavinusuru vituo vya kuzalishia umeme na hatari ya upungufu wa maji ambayo matokeo yake ni kukatikakatika kwa umeme.
“Pamoja na upungufu wa maji tuliojionea katika mabwawa tuliyotembelea hali ya uzalishaji umeme katika vituo vyake hauwezi kusababisha mgao kwa sasa,” alisema.