SHIRIKA la Umeme (TANESCO) limekamilisha mradi wa usambazaji umeme katika kitongoji cha Nyamalapa kijiji cha Lushimba wilayani Nyang’hwale ambapo miongoni mwa wanufaika wakubwa ni wachimbaji wadogo.
Mradi umehusisha ujenzi wa laini ya umeme wa msongo wa kati Kilovati 33, urefu mita 200, msongo mdogo njia tatu Voliti 400 urefu mita 1270, msongo mdogo njia moja urefu mita 340 na kusimika mashine umba moja KVA 315.
Meneja wa Tanesco wilaya ya Nyang’hwale Lucas Karoli amesema hayo katika taarifa yake kwa viongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka 2024.
Karoli amesema ujenzi wa mradi huu ulianza Novemba 2023 na kukamilika Juni 2024 chini ya utekelezaji wa TANESCO Nyang’hwale kwa gharama ya Sh milioni 78.98 ambayo ni pesa kutoka serikali kuu.
SOMA: Tanesco yatakiwa kurekebisha miundombinu Mtwara
Amesema tayari nishati ya umeme imefikishwa katika maeneo nyeti ya uzalishaji mali ambayo ni viwanda vidogo vinavyojihusisha na uchenjuaji wa madini ya dhahabu kitongoji cha Nyamalapa.
Amesema hatua hiyo imepunguza gharama za uendeshaji wa mitambo ya uchenjuaji wa madini ya dhahabu ukilinganisha na matumizi ya mafuta hapo awali.
Mkurugenzi wa Kampuni ya MOSO CO.LTD, Mohamed Masoud amesema kabla ya kupata huduma ya Umeme walikuwa wakitumia mafuta ya dizeli wastani wa Lita 7200 ambapo ni sawa na Sh milioni 24.4 kwa mwezi.
“Baada ya Kupata huduma ya Umeme tunalipa bili wastani wa kiasi cha Sh milioni 2.2 kwa mwezi ambayo ni pungufu ya shilingi milioni 22.2 kutoka kwenye gharama za kununua mafuta ya dizeli.
“Aidha, kabla ya kupata huduma ya Umeme tulikuwa tunazalisha udongo tani 150 hadi 200 kwa mwezi, na kwa sasa wakati tunatumia umeme tunazalisha udongo kiasi cha tani 350 hadi 600,” amesema.
Naye Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame amesema mpaka sasa kata zite 15 na vijiji vyote 62 vya halmashauri hiyo vina umeme, huku kazi ya kufikisha umeme kwenye vitongoji vyote 273 ikiendelea.
SOMA: Dk Biteko avunja bodi kampuni ya Tanesco
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2024, Godfrey Mnzava amewaomba wachimbaji wadogo kutumia fursa ya nishati ya umeme ya uhakika kuongeza kiwango na ubora wa uzalishaji kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.