Tanesco yatakiwa kurekebisha miundombinu Mtwara
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imelitaka Shirika la Umeme (TANESCO) mkoani Mtwara inarekebisha miundombinu ya umeme katika mkoa huo.
Akizungumza leo mkoani Mtwara, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kilumbe Ng’enda amesema wamefanikiwa kuongeza uzalishaji na kuna umeme mwingine wa ziada lakini miundombinu inawaangusha.
Kamati hiyo iko mkoani humo kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na kazi zingine za kuishauri serikali pia kuangalia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) ikiwemo ya gesi asilia iliyopo kijiji cha Msimbati na Madimba kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani humo.
Miradi mingine ya maendeleo iliyotembelewa ni kituo cha afya Msimbati kilichogharimu Sh milioni 700, kituo cha polisi na kupata fursa ya kuzungumza na wananchi wa kata ya Msimbati kwenye halmashauri hiyo walipokuwa katika miradi hiyo ya maendeleo katani humo.
SOMA: Wabunge wasisitiza matumizi ya gesi asilia viwandani
Amesema wanajua kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake katika kuhakikisha mkoa huo unapata umeme wa uhakika.
“Tunajua hiyo kazi na tunampongeza Rais, tunaipongeza serikali, tunafahamu kazi hiyo ni ya tanesco kutwa kucha lakini kwa kuwa sisi tumepita hapa kwahiyo wananchi wa mtwara waseme kamati imepita na msisitizo wake mabadiliko wanayaona,” amesema Ng’enda.
Hata hivyo ameipongeza tanesco kwa kufanikisha kuvifikia vijiji vyote 785 katika mkoa huo kwa kupitiwa na umeme wa Wakala wa Umeme Mijini na Vijijini (REA) kwani ni hatua mzuri na kubwa na ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Tuendelee kupelekea umeme huo vitongojini kama ambayo hatua ya wizara sasa hivi inavyosimami jambo hili,” amesema.
Aidha amewaomba wananchi wa maeneo hayo kuwa, wenye wajibu wa kutunza miradi hiyo ni wao ikiwemo ya gesi asilia ambayo inawanufaisha wananchi wa maeneo hayo na watanzania kwa ujumla.
SOMA: Kamati ya Bunge yasifu uwekezaji gesi Mtwara
Akiwa katika kituo hicho cha afya katani humo, Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amesema fedha iliyojenga kituo hicho ni fedha ya kurudisha kwa jamii iliyotolewa na TPDC
Salma Mohamed mkazi wa kijiji cha msimbati kwenye halmashauri hiyo, ameipongeza Tpdc na serikali kwa ujumla kwa kuwekeza miradi hiyo ya maendeleo ikiwemo kituo hicho cha afya kwani kimewarahisishia upatikanaji wa huduma hiyo kwa urahisi.