ZAIDI ya tani laki 400,000 za korosho ghafi zimeuzwa kupitia minada ya korosho katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025 zenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 1.4.
Hayo yamejiri wakati wa kufunga mafunzo ya siku tano kwa maofisa ugani kuhusu kuwajengea uelewa zaidi kwa namna ambavyo wanaenda kutekeleza majukumu hayo kwenye maeneo mbalimbali mkoani humo, yaliyofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Udhibiti Ubora Revelian Ngaiza amesema tani hizo zaidi ya laki 400,000 za korosho ghafi zilizouzwa katika mismu huo wa mwaka 2024/2025 kupitia minada ni hadi kufikia Januari 3, 2025 ambapo minada ya korosho katika msimu huo wa mwaka 2024/2025 ilifunguliwa rasmi Oktba 11, 2024.
Amesema ni adhima ya serikali kuboresha na kuinua sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo ambapo Cbt imetekeleza programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kwa kuajiri maofisa ugani hao 500 kwa kuanzia na kuwagawa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kata, vijiji ambako wataenda kuwa chachu kwa kusaidiana na wakulima katika kuongeza tija kwenye zao hilo.
Maofisa ugani hao wameajiriwa katika mikoa mitano ya asili inayolima korosho nchini ikiwemo Mtwara, Lindi, Pwani, Ruvuma na Tanga ambapo kati ya hao mkoa wa mtwara wamechukuliwa 245 ambao ni takribani ya asilimia 60 ya maofisa ugani wote waliyochukuliwa.
‘’Miongoni mwa shughuli ambazo wataenda kuanza nazo ni kuboresha kanzidata ya wakulima, tulishafanya kwenye maeneo lakini bado tunahitaji kuboresha kuhakiki yale mashamba kuona tuliyoandika mule kama ni sahihi kwahiyo vijana hawa wanaenda kutekeleza’’amesema Ngaiza
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Benedicto Ngaiza amesema hatua hiyo ni utekelezaji kwa vitendo wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika jitihada za kuendeleza zao la korosho nchini kutokana na machango wa zao hilo wa kuongeza pato kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Amewasisitiza maofisa hao kuwa, serikali imewaamini na kuwapa fursa hiyo na kuwa sehemu ya wataalam katika zao hilo na kupatiwa mafunzo hayo hivyo waende wakatekeleze majukumu hayo kwa ufanisi na bidii kubwa ili waweze kutimiza malengo ya Cbt na serikali hiyo kwa ujumla.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki hao wa mafunzo akiwemo Joha Abdallah ameipongeza serikali kwa kuwaamini na kuwapatia ajira hiyo na mafunzo kwa ujumla ambayo wataenda kuyatendea haki kwa kuhakikisha elimu hiyo wanaifikisha kikamilifu kwa wakulima ili kuwezesha lengo la serikali.