Tanzania, China kuenzi urafiki wa Nyerere

DAR ES SALAAM: Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC) kimeandaa Mbio za Tanzania-China kwa lengo la kuenzi mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, katika kuimarisha urafiki na ushirikiano kati ya Tanzania na China.

Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Oktoba 14, 2026, huku zikilenga kuhamasisha wananchi kuzingatia maisha yenye afya, kuwaleta pamoja Watanzania na raia wa China wanaoishi nchini pamoja na kusaidia huduma za kijamii kupitia fedha zitakazopatikana katika tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa EACLC, Lisa Wang, amesema mbio hizo si kwa ajili ya michezo na afya ya mwili pekee, bali pia ni sehemu ya kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa mchango wake katika kujenga na kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China.

Amesema tukio hilo litawakutanisha Watanzania, raia wa China wanaoishi Tanzania, wafanyakazi wa kampuni za China, taasisi za Serikali, sekta binafsi, vijana, wakimbiaji na wafanyabiashara kwa ajili ya kuadhimisha urafiki, umoja na uhusiano wa watu wa mataifa hayo mawili.

Wang amewataka Watanzania, raia wa China na watu wengine kushiriki mbio hizo pamoja na familia zao, akisema zitatoa fursa ya kufanya mazoezi na wakati huo huo kuadhimisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China.

Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la China katika Benki ya NBC, Linas Kahisha, amesema benki hiyo inashirikiana na EACLC kuunga mkono tukio hilo na kuwataka Watanzania wa rika mbalimbali kujitokeza kushiriki.

Naye, Katibu Mkuu wa Chama cha Makampuni ya China Tanzania, Juma Suluhu, amesema mbio hizo zitakuwa na umbali wa kilomita tano, 10 na 15, huku ada ya usajili ikiwa Sh 35,000 kwa mtu mmoja na Sh 32,000 kwa kila mshiriki kwa makundi yenye watu 10 au zaidi.

Suluhu amesema fedha zitakazopatikana zitatumika kusaidia huduma za kijamii, hivyo kufanya tukio hilo kuwa na manufaa zaidi ya michezo na mazoezi ya mwili.

Aidha, amewataka washiriki kuchagua umbali unaoendana na uwezo wao wa kiafya na kimwili ili kushiriki kwa usalama.

Katibu wa Klabu ya Wakimbiaji, Godfrey Mwanakurya, amewahimiza wananchi ambao bado hawajajisajili kufanya hivyo, akisema njia za mbio kwa umbali wote mitatu tayari zimeandaliwa kwa kuzingatia usalama wa washiriki.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button