Tanzania, Kenya kuimarisha ubia uwekezaji miundombinu

KENYA: Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, amekutana na Waziri wa Baraza la Mawaziri anayesimamia Hazina ya Taifa nchini Kenya, John Mbadi, jijini Nairobi, kujadili mikakati ya kuongeza uwekezaji katika miradi ya miundombinu kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).

Mazungumzo hayo yamejikita katika namna ya kuvutia wawekezaji, upatikanaji wa fedha na kuimarisha ushirikiano wa sekta za umma na binafsi katika utekelezaji wa miradi ya barabara.
Viongozi hao pia wamebadilishana uzoefu kuhusu uandaaji, ufadhili na usimamizi wa miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwamo mifumo ya ulipaji wa huduma za baadhi ya miundombinu ili kuhakikisha miradi inakuwa endelevu na yenye tija.

Mkutano huo umehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Uwekezaji wa Umma na Usimamizi wa Rasilimali za Serikali, Cyrell Wagunda, pamoja na viongozi wa Idara ya PPP nchini Kenya wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Kefa Seda.

Kadogosa na ujumbe wake wapo nchini Kenya kushiriki Mkutano wa 16 wa Afrika kuhusu Ufadhili, Uwekezaji na Ubia katika Miundombinu (Africa PPP 2026), unaofanyika jijini Nairobi na kuwakutanisha wadau wa maendeleo, wawekezaji na taasisi za kifedha kujadili mikakati ya kuongeza uwekezaji katika miundombinu barani Afrika.




