TANZANIA inatarajia kuingiza zaidi ya Sh bilioni 352 kwa mwaka kutokana na uuzaji wa vioo vitakavyozalishwa na kuuzwa nje ya nchi kupitia viwanda viwili vya kigeni kutoka China.
Viwanda hivyo ni Saphier Glass na Keda Glass factory ambapo kwa kila kiwanda asilimia 25 ya uzalishaji wake utakuwa kwaajili ya soko la ndani na 75 zitauzwa katika soko la nje.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Uwekezaji, Dk Tausi Kida amesema hayo Juni 19, 2023 katika ziara yake ya kutembelea miradi ya kimkakati wilayani Mkuranga, mkoani wa Pwani.
Amesema zaidi ya asilimia 80 ya malighafi zitakazotumika zitatoka nchini lakini pia ajira 7,000 zitazalishwa kutoka katika kila kiwanda pindi ujenzi utakapokamilika ambapo hadi sasa zaidi ya watu 850 wameshaajiriwa kupitia ujenzi unaoendelea kupitia viwanda hivyo.
“Tumefarijika uwekezaji huu mkubwa unakwenda vizuri na changamoto zote zilizokuwepo za maji na umeme zimeshatatuliwa ikiwemo zile za ukinzani wa sheria ya fedha na uwekezaji zimepatiwa majibu kupitia sheria mpya ya uwekezaji iliyopitishwa Disemba mwaka jana, hivyo Tanzania na nchi wanachama jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika SADC wanakwenda kufaidika na miradi hii.” Amesema Dk Kida.
Aidha, Dk Kida ameongeza kuwa kiwanda cha Saphier kimewekeza zaidi ya USD milioni 310 na kinataraji kuanza kazi Septemba mwaka huu wakati kile cha Keda uwekezaji wake ni USD milioni 300 huku kikitarajiwa kukamilika na kuanza uzalishaji Januari 2024.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nassir amesema wilaya yake ni miongoni mwa wilaya zenye viwanda vingi lakini hilo haitoshi kuleka tija itakayopatikana kupitia viwanda hivi bila mikakati thabiti katika kuandaa mazingira rafiki ili kushawishi wawekezaji wengi.
“Leo tupo hapa katika kiwanda cha Saphier kiwanda ambacho ni cha kwanza Tanzania na Afrika Mashariki na hii ni katika matokeo ya juhudi na dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais Samia katika kuhakikisha sekta ya uwekezaji inakuwa nchini.” Amesema
Mkuu wa Wilaya huyo ameongeza kuwa wilaya yake imekuwa ikipokea fedha nje ya bajeti ili kuimarisha ustawi wa uwekezaji, hata hivyo ameahidi kutoa ushirikiano wa karibu na wizara ya uwekezaji, kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na wadau wa uwekezaji ili kuhakikisha azma ya Rais Samia inafikiwa.