BRUSSELS, Ubelgiji – Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ameendelea na juhudi za kukuza ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia ziara yake ya kikazi mjini Brussels, Ubelgiji.
Katika mikutano iliyofanyika Aprili 15, 2025, Waziri Kombo amesisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha uhusiano wa kibiashara, uwekezaji na maendeleo endelevu.
Ameeleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira bora ya biashara kwa kufanya maboresho ya sera na sheria ili kuvutia mitaji ya kigeni na kuimarisha ukuaji wa uchumi. Sekta zilizowekwa mbele katika ushirikiano huo ni pamoja na kilimo, utalii, viwanda, miundombinu, teknolojia, uchumi wa buluu na sekta binafsi.
Miongoni mwa viongozi waandamizi wa EU waliofanya mazungumzo na Waziri Kombo ni pamoja na Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya, Kaja Kallas, Bi. Theodora Gentzis, Makamu wa Rais wa Bunge la EU, Younous Omarjee na Bw. Koen Doens kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Umoja huo. Viongozi hao wamepongeza hatua zinazochukuliwa na Tanzania na kuahidi kuendeleza ushirikiano ili kufanikisha maendeleo ya kweli kwa wananchi.
Mbali na ushirikiano wa kiuchumi, ziara hiyo pia inalenga kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kisiasa kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, ambao ni miongoni mwa washirika wakuu wa maendeleo ya nchi.
