Tanzania itashirikiana na nchi nyingine za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili kuboresha huduma za Mawasiliano ikiwemo kupunguza gharama za mawasiliano (roaming costs) miongoni mwa nchi wanachama.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa pili wa Kamati ya Udhibiti wa Uchumi (ERC) ya Chama cha Wadhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA) ulioratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi-Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Khalid Mohamed alisisitiza kuwa Serikali itatathmini pendekezo la CRASA juu ya kupunguza gharama za Mawasiliano kwenye ukanda wa SADC.
“Kuhusu suala la roaming kama ulivyolizungumzia Mwakilishi wa Katibu Mtendaji wa CRASA, sisi pamoja na wenzetu tutaangalia namna ambavyo tutaweza kulitekeleza suala hilo ili kuwezesha wananchi wetu kupata gharama nafuu za Mawasiliano wanapokuwa kwenye nchi wanachama wa SADC,” alisisitiza.
Mkutano huo unaofanyika kwa siku Tano utatanguliwa na Semina inayolenga mbali na mambo mengine kuwajengea washiriki uwezo katika ukusanyaji, uchambuzi na utoaji taarifa za viashiria vya ukuaji wa sekta ya Mawasiliano, chini ya uwezeshaji wa Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU).
Akizungumzia ajenda za vikao hivyo Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dk Jabiri Bakari alibainisha kuwa wajumbe wa CRASA watapata fursa ya kuelewa masuala muhimu katika ukuzaji sekta ya Mawasiliano, na kwamba TCRA kama mwanachama hai wa CRASA itapata uelewa wa masuala muhimu yatakayosaidia usimamizi Madhubuti wa gharama za Mawasiliano.
“Huu ni Mkutano muhimu sana na tunatarajia washiriki wote tukiwemo TCRA kurejea nyumbani tukiwa tumeshibishwa elimu katika maeneo bayana.
Ikumbukwe kwamba kwenye Mkutano huu, washiriki watajengewa uwezo kuhusu upangiliaji gharama za vifurushi vya mawasiliano ili kuongeza uelewa wa nchi wanachama hatimae kukuza ufanisi wa utoaji huduma za Mawasiliano katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na sisi hapa kwetu tutanufaika sana,” aliweka bayana Mkurugenzi Mkuu wa TCRA.
Nae Kaimu Katibu Mtendaji Mkuu wa CRASA Bwana Shukya Kiroga, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Kielektroniki wa CRASA, akizungumzia hatua zilizofikiwa katika kuhakikisha nchi wanachama wa CRASA zinafikia muafaka kuhusu kulinganisha masharti ya gharama za huduma za Mawasiliano alisema kuwa, utafiti wa kitaalamu wa gharama elekezi tayari umekamilika na kinachotakiwa sasa ni nchi wanachama kuanza utekelezaji.
Aidha, alitoa angalizo kwamba Utekelezaji unahitaji makubaliano ya nchi wanachama ili kufanyika bila mkwamo wakati Utekelezaji wake utakapoanza.
“Ni muhimu sana nchi wanachama wote wakakubaliana, sisi kwa upande wetu tumetekeleza wajibu wetu kinachosubiriwa ni nchi wanachama waridhie kisha Utekelezaji wake uanze, hii nikiamini itapunguza pakubwa gharama za Mawasiliano kwenye ukanda wa SADC,” aliongeza.
Chama cha Wadhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA) kinazileta pamoja Mamlaka Kumi na Tatu za Usimamizi wa Mawasiliano Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo ni Tanzania (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Zambia (Mamlaka ya Habari na Teknolojia ya Mawasiliano (ZICTA), Zimbabwe(Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Posta (POTRAZ), Afrika Kusini (Mamlaka Huru ya Mawasiliano (ICASA).
Msumbiji (Taasisi ya Taifa ya Mawasiliano (INCM), Namibia (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Namibia (CRAN), Eswatini (Kamisheni ya Mawasiliano (ESCCOM) na Malawi (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Malawi (MACRA).