Tanzania mwenyeji Tuzo za 32 Utalii

DAR ES SA SALAAM; Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Tuzo za 32 za Kimataifa za Utalii kwa Ukanda wa Afrika na Bahari ya Hindi zinazotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Juni 28 mwaka huu.
Akizungumza kuhusu tuzo hizo Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru alisema hizo ndiyo tuzo kubwa zaidi za utalii ambazo zinafanyika kwa kanda ya Afrika na Tanzania imepewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa tuzo hizo mwaka huu na takirbani wageni 500 wa ndani nan je wanatarajiwa kuhudhuria.
“Tanzania imekuwa ni nchi pekee katika Afrika kwa mwaka huu kuandaa tukio hili, nchi nyingine ni pamoja na Mexico Italia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Baghrain ambao wanafanya kwa kanda zao na baadaye tukio la dunia litatangazwa na wanaoandaa,” alisema.
Alisema tuzo hizo zinazoandaliwa na Kampuni ya World Luxury Media Group, zina lengo la kutambua wadau walio katika sekta ya utalii na mchango wao katika sehemu mbalimbali na pia ni nafasi kwa Tanzania kuonesha mazao mbalimbali ya utalii.
Mafuru alisema wadau mbalimbali wa utalii watawania tuzo hizo wakiwemo bodi mbalimbali za utalii, watoa huduma za malazi, vivutio mbalimbali vya utalii, watoa huduma za usafiri wa anga, usafiri wa ardhini, kampuni bora za meli za kitalii, kampuni bora za usafiri wa treni za kitalii pamoja na kampuni mbalimbali zinazoendesha shughuli za utalii wa mikutano na matukio.
Alisema mpaka sasa jumla ya wadau 50 wanawania tuzo hizo mwaka huu, 38 wakiwa ni kutoka sekta binafasi na 12 kutoka taasisi za serikali.
Alisema mwaka jana tukio hilo lilifanyika ilifanyika Mombasa, Kenya na Tanzania ilishinda tuzo tano ikiwa inaongoza kwa kupata tuzo nyingi.
Alizitaja tuzo hizo kuwa ni Bodi Bora ya Utalii Afrika ambapo TTB ilichukua, Kivutio Bora Utalii Afrika (Mlima Kilimanjaro), Hifadhi Bora ya Taifa Afrika (Serengeti), Kivutio Bora cha Safari Duniani na katika ngazi ya afrika Tanzania iliongoza kwa kutembelewa zaidi.
Alitoa rai kwa wadau wa sekta ya utalii walio Dar es Salaam watumie fursa zitakazojitokeza katika kuwahudumia wageni watakaohudhuria ikiwemo usafiri, malazi, burudani na chakula.
Meneja Mkuu wa Hoteli ya Johari Rotana ambao ndiyo Hoteli washirika wa tukio hilo, Ahmed Said, aliishukuru TTB kwa fursa ya kuandaa na kusimamia tukio hilo na kusema kuwa wako tayari na wamejitoa kuwapokea na kuwahudumia wageni hao kwa uhakika na umakini.
Naye Meneja Masoko wa hospitali ya Shifaa ya Dar es Salaam, Victoria tarimo ameihakikishia TTB kwamba wamejiandaa vyema kuwapokea na kuwahudumia wageni hao kwa dharura yoyote ile na wana vifaa vya kutosha, vya kisasa vyenye ubora wa kimataifa. Hospitali hiyo ni washirika wa huduma za afya katika tukio hilo.