Tanzania, Namibia zasaini hati za ushirikiano

TANZANIA na Namibia zimesaini hati za makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya usalama, mishati na mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia.

Hati za Makubaliano hayo zimesainiwa katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Tanzania na Namibia uliomalizika jijini Windhoek, Namibia, Machi  10, 2023 katika ngazi ya mawaziri.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax, ambaye ameambatana na Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, David Silinde na Naibu Waziri Nishati, Steven Byabato.

Kwa upande wa ujumbe wa Namibia umeongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Dk  Netumbo Nandi-Ndaitwah, ambaye aliambatana na Mawaziri wa kisekta na Makatibu Wakuu wa nchi hiyo.

Mkutano wa Tatu wa JCC kati ya Tanzania na Namibia umejadili na kutathimini masuala mbalimbali ya utekelezaji kwenye maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa baina ya nchi hizo.

Maeneo hayo ni pamoja na Siasa na Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Uchumi, Nishati, Kilimo, Maendeleo na Miji, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Maliasili, Utalii na Mazingira,  Uvuvi, Afya, Elimu na Utamaduni.

Mkutano huo Mawaziri umewaagiza watendaji katika sekta za ushirikiano kukamilisha kwa wakati masuala yote yanayohitaji utekelezaji ndani ya muda ulioazimiwa na kikao hicho, ili kuleta tija katika shughuli za wananchi na kuwainua kiuchumi.

Vilevile, wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Bara la Afrika kwa ujumla.

Wakihutubia katika ufunguzi wa mkutano huo Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Namibia,  Dk Stergomena Tax na Dk  Netumbo Nandi-Ndaitwah, wamesisitiza umuhimu wa kukuza mawasiliano baina nchi hizo mbili ili kuweza kurithisha kizazi cha sasa juu ya historia ya mataifa hayo mawili na kufahamu ndoto kubwa waliyokuwa nayo waasisi wa matifa haya katika kuyafikia maendeleo ya watu wake.

 

Habari Zifananazo

Back to top button