TANZANIA ikiwa ni miongoni mwa nchi ambazo ziko hatarini kupata ugonjwa wa polio leo nchi sita za Ukanda wa Afrika wamekutana kujadili mikakati ya kutokomeza ugonjwa huo.
Nchi za jirani ambazo bado zinakabiliwa na ugonjwa huo ni DR Congo, Msumbiji, Kenya, Uganda na zingine.
Akizungumza katika mkutano wa 34 wa siku nne wa Ukanda wa Afrika wa kutokomeza ugonjwa wa Polio jijini Dar es Salaam, mratibu wa kutokomeza polio Kanda ya Afrika, Jamal Ahmed amesema lengo kubwa ni kuangalia kuhusu kutokomeza ugonjwa huo kwa kuangalia wamefika wapi na mikakati ya kwenda mbele zaidi.
“Virusi hivi huwa vinavuka mipaka kazi yetu ni kujadili hatari hiyo na kuungana kama majirani kwa juhudu zetu nchi moja pekee haiwezi kumaliza kwasababu kuna mwingiliano na tunataka Disemba mwaka 2025 tuwe tumemaliza,”amesisitiza.
Ameongeza “Hapa tutajadili kuwalinda watoto wa Tanzania na nchi zingine mwisho wa mkutano huu tutakuwa na makubaliano itakayosaidia nchi kuchukua hatua ili kuhakikisha mlipuko huu unafika mwisho mwaka 2025.
Mgeni rasmi katika ufunguzu wa mkutano huo wa siku nne ulioanza Oktoba 29 hadi Novemba 1,2024 ,Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Hassan Hafidhi amesema wamepiga hatua kubwa kwa sasa ni nchi isiyokuwa na polio lakini baadhi ya nchi za jirani bado upo.
“Ili tuwe huru lazima majirani zetu hawana ugonjwa huu na tumefika pazuri tunaangali jinsi ya kuhakikisha tutalinda Polio isirejee kabisa na tunataka nchi zote hazina polio hivyo tunajadili mikakati zaidi na tunahitaji fedha zaidi ili kuimarisha maabara ili kujilinda na hili.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Kinga Wizara ya Afya, Dk Vida Makundi amesema Tanzania mgonjwa wa mwisho ilikuwa mwaka 1996 na kuanzia hapo ugonjwa ulizuiliwa.
“Tunaendeleza kufuatili lakini hatuna mgonjwa ila tunafanya ufutiliaji wa watoto chini ya miaka 15 akipooza tunachukua sampuli kuangalia kama anapolio,tunachukua sampuli katika mazingira tuone kama yamechafuliwa pia tunaangalia katika mipaka.
Amesema pia wanafanya ufuatiliaji wa dalili za ugonjwa wa Polio,kutoa chanjo kwa watoto na wanatoa ujumbe kwa jamii kuendelea kujikinga kwa kuweka mazingira safi.
“Tutawaelezea wenzetu mikakati tuliyoweka na wao wajifunze na sisi tutajifunza kutoka kwao tunaweka nguvu za pamoja kuhakikisha dunia haina Polio 2030.
Naye Kiongozi wa huduma za chanjo na ufuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO)DK Wiliam Mwengee ameeleza kuwa mwaka 2015 Tanzania ilipata cheti cha kuonesha haina polio.
“Tumepewa kazi ya kusaidia nchi kitaalamu na kifedha kwanza kuhakikisha uchanjaji kwa watoto wote pili kampeni za chanjo ili kupata watoto wote tulifika kila mahali tatu ni ufuatiliaji wa watoto waliopooza ghafla kwa kuwapima.