SERIKALI ya Tanzania na Uturuki zimekubaliana kushirikiana kukuza sekta ya maliasili na utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchi hizo mbili.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Dk Mehmet Gulluoglu wamezungumza hayo leo Novemba 19, katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni ushirikiano kati ya Bodi za Utalii za Tanzania na Uturuki katika utangazaji wa maeneo ili kuongeza watalii, kushirikiana na Shirika la Ndege la Uturuki kwa ajili ya kukuza na kuhamasisha watalii kuelekea Tanzania na kuanzisha ubia kwa matukio ya kimataifa ya utalii ambayo Bodi ya Utalii Tanzania inaandaa au kushiriki ikiwa ni pamoja na maonyesho ya Swahili International Tourism Expo (S!TE).
Waziri Chana alitumia fursa hiyo kunadi maeneo ya uwekezaji ya Tanzania na kukaribisha wawekezaji kutoka Uturuki kuwekeza katika huduma za malazi, usafiri na utalii, mashirika ya ndege, biashara ya uendeshaji wa utalii, vituo vya mikutano na uwindaji wa kitalii.
“Napendekeza Tanzania na Uturuki kukuza ushirikiano kati ya sekta binafsi ya nchi hizo mbili ili kuweza kufanya kazi kwa pamoja katika masuala ya biashara ya utalii na uwekezaji,” Chana amesisitiza.
Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Dk Mehmet Gulluoglu amesema Uturuki iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kukuza Sekta ya Maliasili na Utalii huku akisisitiza kuwa Tanzania inavutia na imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii.