Tanzania yaadhimisha siku ya usafiri majini

DAR-ES-SALAAM : TANZANIA leo imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Usafiri Majini Duniani, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed Salum, ametoa wito kwa jamii kulinda mazingira ya bahari.
Amesema kaulimbiu ya mwaka huu “Bahari Yetu, Wajibu Wetu, Fursa Yetu” inakumbusha umuhimu wa bahari katika kutoa ajira, kuchochea uchumi na kuhifadhi uhai wa viumbe majini. SOMA: Mamlaka za usafiri majini Afrika zatakiwa kushirikiana
Amesema shughuli za kibinadamu zimeathiri kwa kiwango kikubwa uwezo wa bahari kutekeleza majukumu yake, akitaja uchafuzi wa plastiki, kumwagika kwa mafuta, kemikali, uvuvi kupita kiasi na ongezeko la hewa ya ukaa kuwa changamoto kubwa. Ameeleza hali hiyo inachangia ongezeko la joto duniani, kupanda kwa maji ya bahari na kuathiri maisha ya jamii nyingi hasa visiwani.
Salum amesisitiza kulinda bahari ni wajibu wa pamoja kwa serikali, sekta binafsi na wananchi. Amesema hatua madhubuti zinahitajika kupunguza uchafuzi, kuhimiza usafirishaji endelevu na kukuza uchumi wa buluu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.