Tanzania yaandaa chuo umahiri wa usafiri wa majini

DAR ES SALAAM: Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema Chuo Kikuu cha Kikanda cha Usafiri kwa Njia ya Maji (RMU) kinatarajiwa kujengwa Tanzania ili kuwa kitovu cha elimu, mafunzo, utafiti na ubunifu katika sekta ya usafiri wa majini kwa nchi wanachama wa Shirika la Bahari la Kanda ya Mashariki, Kusini na Kaskazini mwa Afrika (MOESNA).

Kihenzile amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na MOESNA pamoja na nchi wanachama kuhakikisha chuo hicho kinakuwa kituo cha umahiri wa kikanda kitakachosaidia kuandaa wataalamu wenye ujuzi wa kukabiliana na mahitaji ya sekta ya usafiri wa majini.

Akizungumza na vyombo vya habari kuhusu maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 10 wa Baraza la Mawaziri la MOESNA, alisema uwekezaji katika miundombinu ya bandari na meli unapaswa kwenda sambamba na kuimarisha rasilimali watu, teknolojia na mifumo ya usalama.

“Miundombinu bila ujuzi haiwezi kutoa manufaa yake kikamilifu, teknolojia bila wataalamu waliopata mafunzo haiwezi kuleta matokeo endelevu,” alisema.

Amesema chuo hicho kitakuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha elimu, mafunzo, utafiti na ubunifu, huku kikijenga kizazi kipya cha wataalamu watakaosaidia kukuza usafiri wa majini na biashara barani Afrika.

Kihenzile aliongeza kuwa maendeleo ya sekta hiyo hayawezi kutegemea uwekezaji katika bandari, meli na miundombinu pekee, bali yanahitaji pia wataalamu wenye weledi katika usimamizi, udhibiti, usalama na ulinzi wa shughuli za majini.

Amesema Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 10 wa Baraza la Mawaziri la MOESNA utakaofanyika Oktoba 15, mwaka huu, ukitarajiwa kuhudhuriwa na takribani mawaziri 26 wanaosimamia masuala ya uchukuzi na lojistiki kutoka nchi wanachama, pamoja na wawakilishi wa taasisi za kikanda na kimataifa.

Amesema ajenda muhimu ya mkutano huo ni kujadili namna ya kukuza biashara kwa kupanua usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya meli kati ya bandari za Afrika, pamoja na kuweka mazingira wezeshi yatakayoongeza ushiriki wa nchi za Afrika katika biashara ya kikanda na kimataifa.

Aidha, amesema mkutano huo utajadili namna ya kuhamasisha uanzishwaji wa mashirika ya meli ya Afrika yatakayoshirikiana na makampuni makubwa ya usafirishaji wa majini duniani ili kuiunganisha Afrika na masoko ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Kihenzile, hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uwekezaji katika sekta ya usafiri wa majini, kufungua fursa za ajira kwa vijana na mabaharia, pamoja na kuimarisha biashara baina ya nchi wanachama.

Amesema kuwa usafiri wa majini ni nguzo muhimu ya uchumi wa Afrika, akieleza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya biashara ya nje ya bara hilo husafirishwa kwa njia ya bahari, huku zaidi ya asilimia 80 ya biashara ya bidhaa duniani kwa ujazo ikifanyika kwa njia hiyo.

Amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuwa na bandari zenye ufanisi, huduma bora za meli na mifumo ya usafirishaji inayounganisha bandari na maeneo ya uzalishaji, viwanda na masoko.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) na Ajenda ya Afrika 2063 unahitaji mifumo madhubuti ya uchukuzi na lojistiki ili kuongeza biashara baina ya nchi za Afrika, kukuza viwanda na kuimarisha ushiriki wa bara hilo katika minyororo ya thamani ya uzalishaji ya kikanda na kimataifa.

Akizungumzia nafasi ya Tanzania katika sekta hiyo, Kihenzile amesema nchi imejaliwa kuwa na nafasi ya kimkakati katika Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, hali inayoipa wajibu wa kuwezesha biashara kati ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini na masoko ya dunia.

Amesema Bandari ya Dar es Salaam inahudumia takribani asilimia 90 ya biashara ya kimataifa ya Tanzania, huku pia ikitoa huduma kwa nchi zisizo na mwambao wa bahari, zikiwemo Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi na Uganda.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button