Tanzania yaivutia Afrika uwekezaji sekta ya nishati

CAPE TOWN, AFRIKA KUSINI: Tanzania imewaalika wawekezaji kutoka nje kuwekeza katika sekta ya nishati kwa kuwa kuna fursa mbalimbali.

Akiwasilisha mada leo, Novemba 5, 2024, katika Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika unaoendelea nchini humo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi, Dk James Mataragio alibainisha fursa zilizopo katika sekta hiyo kuwa ni vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia, miundombinu ya mafuta na gesi, miradi ya nishati jadidifu na viwanda vya petrokemikali.

Kwa upande wa vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia, Dk Mataragio alieleza kuwa tayari Wizara imekamilisha maandalizi muhimu kuelekea tukio la uzinduzi wa duru ya tano ya kunadi vitalu vya mafuta na gesi asilia vilivyo wazi ambao utaanza rasmi Machi, 2025 wakati wa Mkutano na Maonesho ya Petroli ya Afrika Mashariki utakaofanyika jijini Dar es Salaam.

Advertisement

“Tunatarajia kunadi jumla ya vitalu 26 vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini. Kati ya vitalu hivyo, vitalu 23 vipo eneo la baharini na vitatu vipo eneo la Ziwa Tanganyika” alieleza Mataragio.

SOMA: Wizara yaitaka PURA kujipanga utangazaji vitalu vya mafuta, gesi

Pamoja na vitalu hivyo, Mataragio alieleza kuwa ipo fursa kwa wawekezaji kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuendeleza vitalu vya Eyasi-Wembere, Mnazi Bay Kaskazini na Songo Songo Magharibi; vitalu ambavyo TPDC imeendelea kuvifanyia utafiti wa mafuta na gesi asilia.

Kupitia wasilisho hilo, Mataragio alieleza kuwa taarifa za vitalu vyote vitakavyowekwa sokonina vile vinavyoendeshwa na TPDC) zipo hadharini kwa lengo la wawekezaji kuona na kushiriki mnada huo kikamilifu.

Alizitaja taarifa hizo hizo zinahusu hali ya nguvu sumaku ya miamba (magnetic), uzito wa miamba (gravity), mitetemo (2D na 3D) na visima.

Maeneo mengine ya uwekezaji aliyoyataja katika sekta ndogo ya gesi asilia ni uwekezaji katika ujenzi wa vituo vya kujaza gesi asilia kwenye magari na viwanda vya petrokemikali kwa kutumia gesi asilia.

Pamoja na kueleza fursa zilizopo, Dk Matarajio alieleza kuwa Serikali imefanya kazi kubwa kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kutekeleza miradi ya kimkakati kama vile Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), hivyo Tanzania ni sehemu sahihi kwa uwekezaji.