Tanzania yapiga hatua za maendeleo miaka 61

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Tanzania imepiga hatua kubwa za maendeleo kisiasa, kiuchumi na kijamii ndani ya miaka 61 ya Muungano, na kuwa mfano bora wa mafanikio ya muungano barani Afrika.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Aprili 25 2025, wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Barabara ya Kibada–Mwasonga, iliyopo Wilaya ya Kigamboni, Mkoa wa Dar es Salaam, kama sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanzania.

“Wananchi wa pande zote mbili za Muungano wanaendelea kunufaika na matunda ya Muungano tangu kuasisiwa kwake, hali inayodhihirisha dhamira ya waasisi wetu ya kuleta uhuru, umoja na maendeleo kwa Watanzania,” amesema Dk Mwinyi.

Aidha, Rais Mwinyi alizitaka Wizara ya Ujenzi pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaokubalika, kama ilivyoainishwa kwenye mkataba.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia, Jerry Slaa, alisema kuwa barabara hiyo itafungua fursa za kiuchumi katika Wilaya ya Kigamboni na kuwaunganisha wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameshukuru kwa niaba ya wakazi wa Kigamboni na kupongeza juhudi za serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika unaovutia wawekezaji.

Chalamila aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuitunza miundombinu hiyo muhimu, huku Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, akibainisha kuwa hadi sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 30 na umezalisha zaidi ya ajira 300 kwa wananchi.

“Mradi wa ujenzi wa barabara hii utagharimu Sh bilioni 83.8 hadi kukamilika kwake na unatekelezwa na Kampuni ya Estim Construction Limited,” amesema Mhandisi Besta.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button