DAR ES SALAAM – WADAU wa soka nchini wameisifu Tanzania kupanda kwenye viwango vya ubora vinavyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). Kwenye viwango vya ubora vya Novemba vilivyotolewa juzi, Tanzania imepaa mpaka nafasi ya 106 kutoka nafasi ya 112 iliyokuwepo mwezi uliopita.
Ushindi wa Taifa Stars wa bao 1-0 dhidi ya Guinea, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Novemba 19 ulioipeleka timu hiyo kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Morocco mwakani unatajwa kuchangia Tanzania kupanda kwenye ubora huo wa viwango.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau hao waliisifu Tanzania hasa Taifa Stars kwenye kupanda kwenye ubora huo wa viwango.
“Ni jambo zuri na kiashiria cha soka letu kukua, ni muhimu sana kuendelea kupambana ikiwezekana kupanda zaidi kwenye ubora huu wa viwango vya Fifa,” alisema kiungo wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua.
SOMA: Yanga kujiuliza kwa Namungo leo
Chambua aliungwa mkono na mchambuzi mahiri wa soka wa Azam Media, Ramadhan Mbwaduke aliyesema kupanda kwa viwango vya ubora wa Fifa kutasaidia wachezaji wa Tanzania kucheza kwenye ligi kubwa Ulaya.
“Hii ina faida nyingi kwa soka letu, kubwa sasa wachezaji kama tutaendelea kupanda hivi na kushika nafasi nzuri zaidi, watapata nafasi ya kucheza ligi kubwa za Ulaya.
Baadhi ya ligi hawachukui wachezaji kutoka nchi zilizo kwenye viwango vya chini vya ubora wa Fifa,” alisema Mbwaduke. Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage pia aliisifu Tanzania kupaa kwenye ubora huo wa viwango vya Fifa na kushauri jitihada zaidi ziliendelee kufanyika kuendelea kushika nafasi nzuri zaidi kwenye ubora huo.
Rekodi kubwa zaidi Tanzania kuwahi kushika kwenye ubora wa viwango vya Fifa ilikuwa mwaka 1995 iliposhika nafasi ya 65.