Tanzania yashiriki mkutano wa ITU PP22
ULIMWENGU Habari na Teknolojia ya Mawasiliano, unakutana mjini Bucharest, Romania kuanzia leo Septemba 26, 2022 hadi Oktoba 14, 2022, wakati wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Umoja wa Mawasiliano 2022 (ITU PP22).
Tanzania imewakilishwa kikamilifu katika Mkutano huo na ujumbe wa viongozi wa sekta ya TEHAMA wakiongozwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, ambaye anatarajiwa kuwasilisha tamko la kisera la Tanzania Sptemba 29, wakati wa Mkutano Mkuu huo.
Akizungumza mapema kabla ya mkutano huo, Dk. Jim Yonazi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, amesema Tanzania inashiriki mkutano huo wa PP22 kwa sababu mahususi.
“Tunalenga kuiweka Tanzania katika nyanja ya maendeleo ya TEHAMA duniani na kukuza ushawishi wake kama kitovu cha TEHAMA katika ukanda wa Kati na Kusini mwa Afrika, ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayofanyika kila siku duniani kote,” alisema Dk. Yonazi.
Alisema Tanzania itautumia mkutano huu kuhakikisha inanufaika na mpango mkakati mpya wa ITU unaolenga kuleta muunganisho wa mawasiliano kwa wote na mabadiliko endelevu ya kidijitali.
Pia kushawishi na kuvutia miradi ya kimataifa, kampuni na washirika wa maendeleo katika TEHAMA, ili kujenga uwezo na kukuza ubunifu wa vijana kutumia teknolojia zinazoibuka katika nchi yetu.
Mkutano Mkuu wa ITU “Plenipotentiary” inawaleta pamoja wawakilishi wa nchi wanachama 193 wa Umoja huo.
Mkutano huu ni chombo cha juu zaidi cha kutengeneza sera cha Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU). Hufanyika kila baada ya miaka minne, ni tukio muhimu ambalo nchi wanachama wa ITU huamua juu ya jukumu la baadaye la umoja, na hivyo kuamua uwezo wa shirika kushawishi na kukuza maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) duniani kote.
Akiwakaribisha wajumbe kwenye Mkutano wa 21 Plenipotentiary huko Bucharest, Katibu Mkuu wa ITU, alisema Mkutano huu utakuwa wa kihistoria.
“Nchi wananchama zitaungana katika Mkutano Mkuu wa ITU Plenipotentiary 2022, ili kuweka mwelekeo wa mabadiliko ya kidijitali kwa miaka ijayo, kwa manufaa ya sayari yetu na ubinadamu.” Katibu Mkuu wa ITU alisema katika taarifa yake.
Mkutano huo unaweka sera za jumla za umoja huu, hupitisha mipango mikakati na fedha ya miaka minne na kuchagua viongozi waandamizi wa umoja, nchi wanachama wa Baraza, na wajumbe wa Bodi ya Kanuni za Redio.
Katika Mkutano huu, Tanzania inagombea kuwa mjumbe katika Baraza la ITU, kwa kipindi cha 2023 hadi 2026. Kuna wagombea 17 wa nafasi 13 za Afrika katika Baraza.