Tanzania yatabiriwa makubwa Azimio la Dar

TANZANIA inatarajiwa kufanya makubwa kwenye sekta ya ajira na uwekezaji kutokana na Azimio la Dar es Salaam katika mkutano wa nishati wa Misheni 300 uliomalizika Dar es Salaam Januari 28.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi na wadau wa nishati wamesema mkutano huo na azimio hilo ni fursa kwa Tanzania kwani itazidi kufungua uchumi wa nchi.

Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano huo wa siku mbili Dar es Salaam ulioshirikisha wakuu wa nchi za Afrika Januari 27 na 28.

Advertisement

Katika mkutano huo wakuu wa nchi 12 za Afrika walisaini Azimio la Dar es Salaam kwa lengo la kutekeleza mipango ya kitaifa ya nishati kwa mwaka 2025-2030.

Katika azimio hilo lenye vipengele 15 viongozi hao wamedhamiria kuhakikisha wananchi milioni 300 katika nchi hizo wanapata umeme na nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu na endelevu.

Nchi zilizosaini azimio hilo ni Tanzania, Chad, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Liberia, Madagascar, Malawi, Mauritania, Nigeria, Zambia, Niger na Senegal.

Rais Samia Suluhu Hassan alisema Azimio la Dar es Salaam litakuwa chachu ya ukombozi wa kiuchumi Afrika.

Kwa upande wake mchambuzi wa masuala ya uchumi, Walter Nguma alisema Azimio hilo lina faida kwa Tanzania kwani ni moja ya nchi za Afrika zinazofanya vizuri kwenye nishati ya umeme.

“Tuna zaidi ya megawati 3000 lakini kwa matumizi ya Tanzania ni takribani megawati 1,800 hivi kwa hiyo tuna umeme wa ziada kuuza nje, hii itatusaidia kupata nafuu ya umeme kwani tukiuza vizuri itatuletea mapato,” alisema Nguma.

Aliongeza: “Viwanda vitajengwa na hapa tunaona sekta binafsi inaendelea kualikwa kufanya uwekezaji itafungua
mipaka na sisi (Tanzania) tutakuwa na bidhaa sokoni tunauza umeme.”

Kuhusu mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan kutumia Sh trilioni 33 kuwekeza kwenye umeme Nguma alisema, “Usione vyaelea vimeundwa… hii ndio maana yake, tunataka biashara ya umeme, lazima tuwekeze, nina hakika rais amepata ushauri mzuri ndio maana ameingia kuwekeza, wote walioendelea kwenye biashara hii waliwekeza na rais anawekeza sasa, kupanga ni kuchagua, kama fursa imeonekana kwenye nishati hakuna budi kuitumia.

“Ili uendelee unahitaji kuwa na nishati ya uhakika, nchi zote zenye maendeleo zina nishati ya uhakika na waliwekeza kwenye hilo, uchumi utakua na unajua diplomasia ya uchumi ina nafasi kubwa sana katika kuunganisha mataifa hata Umoja wa Ulaya mambo ya uchumi ndiyo yaliunganisha”.

Alisema nishati ya umeme itakapokuwa ya kutosha Tanzania na bara la Afrika litakuwa na viwanda vya uhakika na watu wake watapata ajira.

“Watu ambao hawana umeme wakifikiwa itakuwa faida kubwa, lakini pia kwa kutumia nishati safi ya kupikia, pia tutatunza na kulinda mazingira yetu Afrika.

“Azimio zuri sana, ila tu tahadhari wasije kwenda kinyume na vile walivyokubaliana… maazimio haya yakienda kama yalivyo Tanzania na Afrika tutapiga hatua kubwa sana, nchi za Afrika zitafanya biashara ya pamoja na kuwa ile Afrika ya mwaka 2063 tunayoitamani kuifikia,” alisema.

Naye Mhadhiri na Mkuu wa Idara Msaidizi Idara ya masomo ya biashara na rasilimali watu Chuo Kikuu Katoliki
cha Mbeya (CUoM), Samson Mwigamba alisema mkutano huo kwa ujumla una manufaa kwa Tanzania kwani
umeme utakapokuwa wa kutosha gharama za uzalishaji zitapungua.

“Ni tofauti na asiyekuwa na nishati ya umeme, hata mfano tizama Treni ya Kisasa (SGR) na ile ya jirani zetu Kenya wao wanatumia mafuta, unaona uzalishaji wao ni tofauti na wetu, sisi tuko juu.

“Faida ya pili kwenye mazingira, ili uchumi uendelee lazima ukue bila kuathiri mazingira, nishati safi itaweka
mazingira safi hatutakata miti hovyo na tutavutia watalii kwani mbuga zetu hazitakuwa kame. Nimefurahia
uwekezaji mkubwa unaokwenda kufanywa na uchumi nao unapanda,” alisema.

Naye Profesa Haji Semboja, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi na fedha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam alisema, “Tanzania itanufaika kwa sababu sisi wenyewe ndio Waafrika, pia dunia inataka tubadilike Afrika tutumie nishati kwa maendeleo, iwekwe mipango mikakati mizuri ya kututoa tulipo na kusongambele”.

Kwa upande wake, Profesa Nyambilila Amuri kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) alisema mkutano wa Misheni 300 una faida kubwa kwani umeme ni kiungo muhimu kwenye matumizi ya kila siku na kutolea mfano sekta ya elimu.

“Pia, itavutia vijana kufanya kazi mahali popote iwe vijijini au mijini sababu ya nishati ya umeme, pia watu wanaweza kujiajiri, pia kuvutia wawekezaji lazima watahitaji nishati kwenye mambo ya kilimo cha umwagiliaji”.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *