Tanzania yatoa wito kwa mataifa tajiri duniani

Yataka yasaidie kukuza uchumi wa nchi zinazoendelea

DODOMA; SERIKALI imezitaka Jumuiya za Kimataifa zisaidie kukuza uchumi wa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ili kupanua wigo wa ushiriki wa wananchi wake.

Hayo yamesemwa leo Novemba 17, 2023 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha tamko la Serikali kwenye ufunguzi wa mkutano wa pili wa Jukwaa la Sauti za nchi zinazoendelea uliofanyika kwa njia ya mtandao chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi.

“Tumeliomba jukwaa hili lione namna ya kushirikisha nchi zinazoendelea kuboresha uchumi wetu ndani ya nchi kwa kukuza biashara na milango ya uwekezaji na namna nyingine zinazoweza kusaidia kuinua uchumi wetu,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Majaliwa ameliomba jukwaa hilo liangalie namna linavyoweza kushirikisha uchumi wa dunia na kuufungamanisha na uchumi wa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Akielezea kuhusu masuala mengine, Waziri Mkuu ameliomba jukwaa hilo lihakikishe linatafuta majibu ya changamoto za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, masuala ya nishati mbadala, uwezeshaji wa vijana na wanawake.

Jukwaa hilo linaziwezesha nchi zinazoendelea kujadili changamoto zinazowakabili na kupaza sauti zao ili ziweze kuwasilishwa kwenye mkutano wa kundi la nchi 20 zenye maendeleo makubwa ya kiuchumi (G20) utakaofanyika Novemba 20, mwaka huu.

Mapema, akifungua mkutano huo, Waziri Mkuu wa India, Bw. Modi alisema licha ya kwamba jukwaa hilo lina wanachama zaidi ya 100, bado wote wanaunganishwa na mahitaji na vipaumbele ambavyo vinafanana.

Mkutano wa leo umeshirikisha wakuu wa nchi na wawakilishi 13.

 

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button