Tanzania yawasilisha mafanikio utekelezaji MEAs

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewasilisha mafanikio yake katika utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa ya Mazingira (MEAs) katika Mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEA-7) unaofanyika jijini Nairobi, Kenya leo Desemba 11, 2025.

Mafanikio hayo yamewasilishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk Festo Dugange kwenye majadiliano ya ngazi ya juu akiwasilisha uzoefu wa Tanzania katika uhuishaji na ukamilishaji wa Mkakati na Mpango wa Taifa wa Uhifadhi wa Bioanuwai (NBSAP).

Katika wasilisho hilo, Dk Dugange amebainisha kuwa Serikali imekamilisha uandaaji wa Mkakati huo uliohuishwa, ukiainisha mwelekeo wa kitaifa katika kutekeleza malengo ya kimataifa ya uhifadhi wa bioanuwai.

Amesema kuwa mafanikio ya mchakato huo yametokana na mbinu shirikishi kupitia uratibu wa pamoja uliohusisha wizara mbalimbali.

SOMA: NEMC yaendesha mafunzo ya nyenzo za usimamizi mazingira

“Uratibu huu umewezesha malengo ya bioanuwai kuingizwa kikamilifu katika mifumo yetu ya mipango ya maendeleo, sera za kisekta na mipango ya taasisi, hivyo kuongeza ulinganifu kati ya vipaumbele vya kitaifa na wajibu wa nchi katika mikataba ya kimataifa ya mazingira,” amesema.

Akifafanua zaidi, amesema mchakato wa NBSAP umeendeshwa pia kwa ujumuishi wa jamii, kwa kuwashirikisha wadau kutoka asasi za kiraia, taasisi za elimu ya juu, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.

Dk Dugange amesema Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Sekretarieti za Mikataba ya kimataifa ya Mazingira pamoja na nchi wanachama, katika jitihada za pamoja za kufikia malengo ya KM-GBF na mikataba mingine ya kimataifa ya mazingira.

“Tanzania ipo tayari kuendelea kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano na kuchangia utekelezaji wa malengo ya kimataifa ya mazingira,” amesistiza Dk Dugange.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button