TANZANIA yazindua tuzo za comedy award

DAR-ES-SALAAM : TANZANIA imezindua rasmi Tuzo za Tanzania Comedy Award kwa mara ya kwanza, lengo likiwa ni kutambua na kuthamini kazi za wasanii wa vichekesho wanaofanya vizuri katika tasnia ya kuchekesha.
Tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika Februari 14, 2025 katika ukumbi wa The Super Dome jijini Dar es Salaam, ambapo wachekeshaji wakongwe na wapya kutoka katika tasnia ya ucheshi watajumuika.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Kampuni ya The Plug na pia msanii wa Bongo Fleva, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ alisema kuwa mshindi wa Comedi Bora ya Mwaka atapata kitita cha Sh Milioni 30. SOMA: Mora mwenyeji tuzo za trace Zanzibar
“Zawadi za mshindi wa jumla wa Best Comedian of the Year atapata kitita cha Sh Milioni 30, huku washindi wengine wa Best Comedian Male na Best Comedian Female kila mmoja akitarajiwa kuondoka na Sh Milioni 20. Mshindi wa kila kipengele atapata Sh Milioni 5,” alisema Dimpoz.
Aliongeza kuwa lengo kuu la tuzo hizo ni kuipandisha thamani tasnia ya ucheshi na kuhakikisha washindi wanapata zawadi zitakazowawezesha kununua vifaa vya kazi zao au kufanya jambo kubwa la kimaendeleo.



