Tarea na Wiki ya Nishati Jadidifu kukomboa jamii

DAR ES SALAAM; “WIKI ya kitaifa ya Nishati Jadidifu Tanzania ina jukwaa la kuonesha teknolojia mpya na suluhisho bunifu za kijamii, kujifunza maendeleo mapya katika nishati jadidifu na ufanisi wa nishati duniani pamoja na kupata maarifa kutoka kwa wataalamu kupitia warsha na semina.”
Anasema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA), Dk Prosper Magali anapozungumzia Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Nishati Jadidifu Tanzania mwaka 2025 (REW2025) yanayofanyika wiki ijayo Mei 26 hadi 29, 2025.
Anabainisha hayo Dar es Salaam hivi karibuni anapozungumzia maadhimisho hayo ambayo mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: ‘Wezesha Uendelevu: Kukuza Matumizi ya Nishati Jadidifu.’
Anasema maadhimisho hayo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam yanatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango Mei 28, na kufungwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko Mei 29, mwaka huu.
“Maadhimisho hayo yanayoandaliwa kwa ushirikiano wa Tarea na Wizara ya Nishati, yanalenga kuunga mkono juhudi za serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kupambana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa na matumizi ya nishati isiyo safi,” anasema.
Kwa mujibu wa Dk Magali, maadhimisho ya mwaka huu pia yanalenga kwenda sambamba na maudhui ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika (Africa Summit 300) uliofanyika Dar es Salaam (Tanzania) Januari 27 na 28, mwaka huu ukiwa na kaulimbiu: ‘Kuharakisha Upatikanaji wa Nishati Afrika’.
Mkutano huo wa kimataifa ulilenga kuimarisha ushirikiano wa Bara la Afrika dhidi ya athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi na kukuza suluhisho la nishati jadidifu.
Lengo Namba 7 la Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa limejikita kuhakikisha kuna upatikanaji wa nishati nafuu, inayopatikana kwa urahisi, endelevu na ya kisasa kwa wote.
Magali anatoa mwito kwa wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo ili kuchangia mustakabali wa nishati Tanzania.
Anasema Wiki ya Nishati Jadidifu si tu ni tukio, bali harakati za kuelekea Tanzania safi, kijani na endelevu zaidi.
Anasema: “Kipaumbele kitatolewa katika kuinua vijana, wanawake na makundi yaliyo pembezoni kushiriki katika miradi ya nishati jadidifu pamoja na kuziba pengo kati ya elimu ya kitaaluma na sekta binafsi, kuhamasisha wanafunzi kuchunguza na kubaini fursa za kazi katika sekta hii inayokua kwa kasi.”
Aidha, anasema tukio hilo ni fursa ya kijamii na kibiashara kwa kuwa litakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwamo mabalozi, sekta binafsi na mashirika ya serikali kama vyuo na vyuo vikuu pamoja na kampuni za ndani na za kimataifa kuunda ushirikiano wa kimkakati na fursa mpya za biashara.

Kwa mujibu wa Tarea, miongoni mwa matukio katika maadhimisho hayo ni ziara maalumu katika kituo cha kuzalisha umeme wa jua mkoani Dar es Salaam na kuonesha matumizi ya teknolojia za kisasa, mafunzo kwa vitendo kuhusu teknolojia mpya za vifaa vya umeme wa jua.
“Kutakuwa na kongamano la siku mbili litakalokwenda sambamba na maonesho ya teknolojia za nishati jadidifu kama upepo, nishati ya jotoardhi, tungamotaka na nishati safi na endeleu za kupikia,” zinasema taarifa hizo.
Taarifa hizo zinaongeza kuwa: “REW2025 itahusisha maonesho ya teknolojia ya nishati jadidifu na matumizi yake kama vile nishati ya jua, magari ya umeme, nishati endelevu za kupikia na teknolojia za ufanisi wa matumizi ya umeme pamoja na ufanisi katika teknolojia za nishati.”
“Wadau wa maendeleo, kampuni binafsi na taasisi za serikali watashiriki kwa kutoa elimu, huduma na kuuza bidhaa mbalimbali za nishati jadidifu kutoka kwa wataalamu wazoefu,” zinathibitisha.
Kwa mujibu wa Dk Magali, kupitia maadhimisho hayo sekta binafsi inatarajia kupata mwongozo kuhusu nafasi (wajibu), fursa na changamoyto za sekta kushiriki kufikia lengo la Watanzania kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia,” anasema.
Anaongeza: “Tunataka tukitoka hapo, serikali nayo ijue nafasi ya sekta binafsi katika mkakati wa kuwafanya Watanzania kuhamia katika matumizi ya nishati safi.”
Kwa mujibu wa Tarea maadhimisho hayo mwaka huu yanadhamiwa na SUNKING, Umoja wa Ulaya (EU) – Expertise France, UNDP, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ENSOL, AG ENERGIES na REX ENERGY.
Mwanzoni mwa mwaka huu wawakilishi kampuni wakandarasi na wauzaji wa vifaa vya umeme utokanao na mionzi ya jua ya ENSOL (T) Ltd, Lameck Kashenshe na Meneja wa Sola wa Kampuni ya Davis & Shirtliff, Saa(T) Ltd da Mandari walinukuliwa na vyombo vya habari wakishuhudia namna kampuni zao zilivyonufaika katika maadhimisho ya Wiki ya Nishati Jadidifu Tanzania Mwaka 2024 ikiwa ni pamoja na kupata teknolojia mpya na kuongeza mauzo ya vifaa na huduma.
Kashenshe alisema kupitia maonesho ya mwaka jana, Ensol Tanzania Limited ilinufaika kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutangaza bidhaa na huduma zao.
Anasema manufaa mengine yalikuwa kujifunza pia kutoka kwa wadau wengine wa nishati jadidifu inayohusisha umeme utokanao na mionzi ya jua, nishati ya jotoardhi, nishati itokanayo na upepo, maji na tungamotaka.
Kuhusu faida za kutumia nishati jadidifu, vyanzo mbalimbali vinasema ni pamoja na ukweli kuwa nishati hiyo (jadidifu) ni rafiki wa mazingira na pia haina madhara kwa watumiaji kwa kuwa haitoi moshi na hewa yenye sumu nyingi inapotumika.
Dk Magali anasema nishati jadidifu hutokana na vyanzo endelevu vinavyopatikana kwa mzunguko kila mahali bila kumalizika ukiwamo umeme.

Akisisitiza umuhimu wa matumizi ya nishati safi anasema, “Nishati safi ya kupikia, ni pale teknolojia inayotumika mfano jiko na chanzo cha nishati vinapotumika kwa pamoja vinapunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha gesi chafu (sumu) kinachozalishwa.”
Anaongeza: “Vyanzo vyote vya tungamotaka, mkaa mbadala, bayogesi ni nishati jadidifu.”
“Kupika kwa umeme ndio teknolojia safi zaidi kuliko zote kwani umeme hauzalishi gesi sumu wakati wa kupika ndio maana tunahamasisha zaidi matumizi ya umeme,” anasema.
Anasema kwa kuwa tayari serikali imefikisha umeme hadi vijijini katika kila kijiji, wananchi wahamasishwe kutumia majiko ya kisasa yanayotumia umeme mdogo na yapatikane kwa urahisi.
Katika dibaji yake kwenye Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034), Naibu Waziri Mkuu na Waziri Wa Nishati, Dk Doto Biteko anasema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni agenda mahususi inayochukua nafasi kubwa katika Sera, Mipango na mikakati ya serikali mbalimbali duniani.
Anasema umuhimu wa agenda hiyo unasukumwa na ongezeko la uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia.
Naibu Waziri Mkuu Biteko anasema, “Hata hivyo, bado kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa nishati nafuu, endelevu na za uhakika kwa matumizi mbalimbali hususani ya kupikia hasa kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania.”
Anaongeza: “Hali hii inasababisha wananchi wengi na baadhi ya taasisi kuendelea kutumia nishati isiyo safi ya kupikia, jambo linaloendelea kuchochea ongezeko la athari za kimazingira, kiafya, kiuchumi na kijamii.”



