Tarura Manyara kufungua barabara mpya Km. 109

WAKALA  ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Manyara ina mpango wa kufungua barabara mpya zenye urefu Km. 109 katika Wilaya ya Mbulu, Simanjiro pamoja na Babati  katika mwaka wa fedha  2024/2025.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja wa Tarura Mkoa wa Manyara, Mhandisi Salim Bwaya wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapo hivi karibuni.

Mhandisi Bwaya amesema kwamba kilomita hizo za barabara zinaenda kuwanufaisha wananchi na kuwaletea manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa kuwarahisishia kupata huduma za kijamii kwa urahisi.

Advertisement

“Mwaka huu wa fedha tuna mpango wa kufungua barabara katika wilaya  ya Mbulu (Km. 46), Simanjiro (Km. 41), pamoja na Babati (Km. 22) ambapo itajumuisha ujenzi wa barabara za lami(Km. 11.7),changarawe (Km. 251.4) pamoja na matengenezo ya barabara za udongo (Km. 385) na ujenzi wa vivuko vipatavyo 104,” amesema.

Amesema kwamba licha ya kufungua kilomita hizo za barabara hali ya mtandao wa barabara katika maeneo mengi katika mkoa huo ni nzuri kwani unapitika katika kipindi chote cha mwaka.

Aidha, amesema kuwa utekelezaji huo unaendelea kutokana na ongezeko la bajeti katika mkoa huo ambapo kwa sasa bajeti yao imepanda mara tatu kutoka Sh bilioni 6.788 mwaka 2021 hadi kufikia Sh bilioni 19.7 mwaka 2024/2025

“Hili ni ongezeko kubwa  na limetuwezesha  kuongeza ubora wa mtandao wetu  wa barabara kwani mwaka 2021 tulikuwa na barabara za lami Km. 17 na sasa tuna Km. 33.03, barabara za changarawe kutoka Km. 950 hadi kufikia Km. 1980 na kiwango kinachobaki ni kiwango cha udongo,” ameongeza.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutuongezea bajeti mara tatu ya  bajeti ya awali na hivyo tumeweza kuongeza madaraja ya mawe kutoka daraja (1) mwaka 2021 hadi kufikia madaraja (10),”.

Pia amesema wameweza kuongeza madaraja madogo na ya kati kutoka 283 hadi 530 vile vile madaraja makubwa yameongezeka kutoka madaraja (2) mwaka 2021 hadi kufikia madaraja (28) kwa mwaka huu wa fedha.

Kwa upande wa mabadiliko ya tabia nchi na utanzaji wa miundombinu ya barabara, Mhandisi Bwaya amesema kwamba wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara yanayosababishwa na uharibifu wa miundombinu hasa mifereji, kung’olewa kwa alama za barabara na uvamizi wa hifadhi za barabara  kwa shughuli za kiuchumi pamoja na umuhimu wa kupanda miti na kutunza mazingira  na kuacha kufanya shughuli zingine za kibinadamu kwenye hifadhi za misitu na kwenye vyanzo vya maji.

Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi  kuendelea kutunza miundombinu ya barabara  kwa kuzingatia  sheria na kanuni zake kwani Serikali inawekeza  fedha nyingi  kwenye miundombinu ya barabara hivyo ni wajibu wao kuitunza ili waendelee kunufaika nayo kwa muda mrefu.

Naye, Mkazi wa Babati, Bakari Sanka amesema Mkoa wao  unapokea mazao mengi kutoka vijijini hivyo kukamilika kwa ujenzi wa madaraja na miundombinu mingine imewanufaisha wananchi wengi na hivyo shughuli zao za uzalishaji zinaendelea kama kawaida.

Pia Hadija Shabani amesema wamefurahi sana kwa ujenzi wa madaraja katika kata zao  kwani makorongo yalikuwa mengi na hivyo msimu wa mvua wanafunzi na watoto walikuwa wakipata shida kuvuka ila kwa sasa imewaokoa na kuwarahisishia usafiri.