Tasac yatoa neno changamoto vijana Ziwa Rwakajunju

VIJANA wanaosafirisha bidhaa zao kutoka nchini kwenda Rwanda kupitia Ziwa Rwakajunju lililopo wilayani ya Karagwe mkoani Kagera wanakutana na changamoto ya kuzuiliwa kubeba bidhaa kutoka Rwanda kuja Tanzania.

Changamoto hiyo imepelekea Bodi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kutoa wito kwa serikali ya Mkoa wa Kagera kuandaa mazingira mazuri kwa vijana hao.

Mwenyekiti wa Bodi TASAC, Nahodha Mussa Hamza Mandia alikiri uwepo wa changamoto hiyo na kwamba vijana wanaotumia Ziwa Rwakajunju lililopo katika mpaka wa Karagwe na Rwanda wanapoleta bidhaa kutoka Rwanda inachukuliwa kama magendo.

Alisema kuwa vijana wengi wanaenda kuuza bidhaa zao Rwanda wakifika wanalipwa faranga na wakifika katika Karagwe wanashindwa kubadilisha fedha hizo na ikitokea wakanunua bidhaa na kuuza Kagera wanakamatwa na mamlaka husika.

“Serikali iangalie pale Mkoa wa Kagera unapoteza pesa, mapato na kila kitu kwanza hakuna sehemu ya kubadili hizo fedha za Rwanda wanahangaika, pili wanachukuliwa kama wahalifu kila wakijaribu kununua bidhaa Rwanda na kuileta Tanzania,”

“Je kuna maaana gani ya kuwa na Jumuiya moja kama hamuwezi kubadilishana uzoefu wa kibiashara na bidhaa ?? serikali lazima itupie jicho pale hiyo ni changamoto.”alisema Mandia

Alisema kuwa changamoto nyingine ni wavuvi kutojua mipaka kati ya mpaka wa Ziwa Victoria upande wa Tanzania na Uganda jambo ambalo linazua migongano huku akitoa wito kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwasa kuhakikisha wanafanya haraka vikao vya ujirani mwema ili kunusuru wavuvi hao pale wanapokuwa wamevuka mipaka.

Aidha bodi hiyo imeuomba uongozi wa mkoa wa Kagera kuanzisha vizimba vya kuzalisha samaki ili kuongeza uchumi wa wakazi wa Kagera pamoja na kujenga barabara nzuri inayoelekea katika mwalo wa magarini.

Hata hivyo alisema pamoja na changamoto hizo ndondogo bado serikali imeshughulikia changamoto nyingi ikiwemo uboreshaji wa mipaka, ujenzi wa miundombinu, uimarishaji wa usalama katika visiwa vya Ziwa Victoria pamoja na ukarabati unaoendelea wa kukarabati kivuko cha Kyenyabasa kinachowavusha wananchi wa Bukoba vijijini.

Habari Zifananazo

Back to top button