Tashico kurejesha huduma za meli kesho

MWANZA: Huduma za meli zinazomilikiwa na Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico) zitarejea kesho Novemba 6, 2025 nchi nzima, baada ya kusimama kwa sababu za kiusalama kufuatia vurugu za hivi karibuni.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu Tashico, Anselm Namala ametoa taarifa hiyo leo Novemba 5, 2025 mkoani Mwanza.
Amesema miongoni mwa meli zitakazorejesha huduma ni pamoja na MV Victoria inayofanya safari zake katika mikoa ya Mwanza na Kagera, kutoka Bandari ya Mwanza Kaskazini, kupitia bandari ya Kemondo hadi bandari ya Bukoba.
Meli zingine ni MV Butiama inayofanya safari zake kati ya Mwanza mjini na Wilaya ya Ukerewe, pamoja na MV Umoja inayosafirisha shehena za mizigo katika bandari zote kubwa za ziwa Victoria kwa Tanzania na nchi jirani.
“Pia huduma zitaendelea katika ziwa Tangayika na ziwa Nyasa. Nichukue nafasi hii kuwafahamisha wateja wetu kuendelea kufurahia huduma hizi kama kawaida,” amesema.



