TASWA wampongeza Waziri wa Michezo
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimepongeza Dk. Pindi Chana kwa kuteuliwa na Rais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo mwanzoni mwa wiki hii.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu wa TASWA, Alfred Lucas leo, imesema pia chama hicho kinampongeza Said Othman Yakub kwa kuteuliwa na Rais Samia kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Uongozi mpya wa TASWA unawaahidi ushirikiano wa kutosha viongozi hao kuhakikisha masuala ya utamaduni, sanaa na michezo yanapata mafanikio makubwa nchini mwetu,” imesema taarifa hiyo.
TASWA pia imezitakia kila la heri timu za Simba, Yanga ambazo wikiendi hii zitakuwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kwa nyakati tofauti kuwakilisha nchi katika michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
“TASWA inaamini Simba na Yanga zitafanya kile ambacho Watanzania wengi tunakitaka wakifanye, nacho ni ushindi, hasa kwa vile watakuwa nyumbani Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
“TASWA inaamini zimejiandaa vya kutosha, zina kila sababu ya kupeperusha vyema bendera ya nchi, tunawasihi mashabiki wote tuziombee timu zetu, kila mmoja kwa imani yake, bila shaka mambo yatakuwa mazuri na hazitatuangusha.
“Pia TASWA inaitakia mafanikio mazuri timu ya Taifa ya Riadha ambayo kesho Jumamosi Februari 18, 2023 itashiriki mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika “World Cross Country Championship’ huko nchini Australia,” amesema Lucas katika taarifa yake.