TAWA waitumia Sabasaba kuhamasisha uwekezaji

DAR ES SALAAM; MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), inatumia maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam kuhamasisha umma wa Watanzania wawekezaji na wageni kutoka mataifa mbalimbali, kuwekeza katika maeneo inayoyasimamia, huku ikitamba kuwa na fursa lukuki za uwekezaji

Akizungumza na wageni waliotembelea banda la TAWA lililopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisa Utalii Daud Tesha amesema TAWA ina uwanda mpana wa fursa za uwekezaji unaotoa mwanya kwa wawekezaji wa aina mbalimbali kuwekeza katika taasisi hiyo

Akizitaja fursa hizo Tesha amesema yapo maeneo mengi yanayohitaji wawekezaji na uwekezaji katika taasisi hiyo, kama vile maeneo ya utalii wa picha kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori, maeneo ya kihistoria yenye utalii wa kiutamaduni, eneo la uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas – SWICA), Uwindaji wa kitalii na ufugaji wa wanyamapori

“TAWA imetenga maeneo kadhaa Kwa ajili ya kufanyika shughuli za utalii wa picha kutokana na ikolojia na aina ya vivutio vilivyopo katika maeneo hayo ikiwemo Pori la Akiba Mpanga/Kipengere eneo ambalo lina maporomoko ya maji zaidi ya 10, ambayo hutoa burudani safi kwa watalii,” amesema Tesha.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/tawa-yatoa-sh-bilioni-9-6-kama-gawio-kwa-vijiji/

“Maeneo mengine ni Pori la Akiba Wamimbiki, Tabora ZOO, Ruhila ZOO , Makuyuni Wildlife Park ambapo wananchi wanakaribishwa kuwekeza kwenye miundombinu ya Utalii ikiwemo kujenga Kambi za Kulala wageni (Campsites), Hosteli, Loji na maeneo ya mapumziko mafupi kwa watalii (Picnic Sites) ameongeza

Kwa upande wake Ofisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wote kutembelea banda la TAWA, Ili kupata maelezo ya fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi hiyo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button