Tawa yafanya usafi kituo cha afya Kingolwira

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imefanya usafi wa mazingira katika kituo cha Afya Kingolwira kilichopo Manispaa ya Morogoro ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali ya maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa usafi katika  kituo hicho cha afya, Ofisa Mhifadhi Mkuu ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhifadhi, Utafiti na Ujirani Mwema, Omary Msangi amesema kuwa hatua hiyo ni kutekeleza  maelekezo yaliyotolewa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Advertisement

Maagizo ya Rais yalitokewa kupitia Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa alipozitaka taasisi zote za serikali kusherehekea maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru kwa kufanya shughuli za kijamii.

“Sisi  TAWA katika kuunga mkono maelekezo ya Serikali tumechagua kufanya usafi kwenye kituo cha Afya Kingolwira na tumefanya  usafi wa mazingira yanayoizunguka kituo hiki,” amesema Msangi.

Msangi ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhifadhi rasilimali za wanyamapori, misitu na mazingira kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kingolwira, Dk Leonard Wambura ameishukuru TAWA kwa kununua vifaa vya usafi  na kufanya usafi wa mazingira katika kituo chao.

” Ninawashukuru TAWA kwa nia yao nzuri ya kuja kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika katika kituo chetu “amesema Dk Wambura. 

Mbali na hayo ameishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha vituo vya afya, na kutoa rai kwa wananchi wa Morogoro  kuendelea kuchangia damu kwa ajili ya kuendelea kuokoa maisha ya mama na mtoto.