TBS yakumbusha kuepuka vipodozi vyenye sumu   

WATANZANIA wameshauriwa kuepuka matumizi ya vipodozi vyenye viambata sumu ambavyo vimepigwa marufuku kutumika nchini kutokana na kusababisha madhara ya kiafya ikiwemo ugonjwa wa kansa.

Ushauri huo ulitolewa na Ofisa Udhibiti Ubora wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Hidaya Kabelege, wakati akitoa elimu kuhusu madhara ya vipodozi vyenye viambata sumu na umuhimu wa usajili wa majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi.

Alitoa elimu hiyo kwenye tamasha la Siku ya Vipodozi 2022 ililofanyika hivi karibuni Dar es Salaam, lililoandaliwa na taasisi ya Tanzania Cosmetology Association.

Kabelege alisema tamasha hilo limekuwa fursa nzuri kwa shirika kutoa elimu ya kwa wananchi juu ya madhara ya vipodozi vyenye viambata sumu na umuhimu wa usajili majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi.

Alisema TBS imekuwa ikitekeleza majukumu hayo kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2019 na kwamba tangu wakati huo imekuwa ikielimisha wananchi kuhusu aina ya vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku na madhara yake.

Kwa mujibu wa Kabelege, kabla ya shirika hilo kukabidhiwa jukumu hilo mwaka 2019, usimamizi wa vipodozi na usajili wa majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi ulikuwa chini ya iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

Alitaja baadhi ya madhara ya vipodozi yenye viambata vya sumu kuwa ni kusababisha ugonjwa wa ngozi na kuathiri ngozi mtumiaji anapokuwa kwenye mwanga. Pia Ngozi huwa laini na kusababisha kupata ugonjwa kama fangasi au maambukizi ya vimelea vya maradhi.

Alitaja madhara makubwa ambayo mtumiaji anaweza kupata ni, kuwashwa kwenye ngozi, kuvimba, ngozi kuharibika, kuchanikachanika,madhara katika mfumo wa uzazi kwa mwanamke na hata kusababisha kupata saratani ya ngozi.

Katika hatua nyingine, Kabelege aliwasisitizia wafanyabiashara umuhimu wa kusajili majengo yao kupitia mfumo unaopatikana kwenye tovuti ya shirika hilo.

Aidha aliwataka wananchi waendelee kutoa taarifa kupitia mawasiliano waliopewa pale wanapogundua uwapo wa bidhaa hafifu katika soko.

Habari Zifananazo

Back to top button