TCAA kamilisheni Ujenzi wa Chuo cha Anga

DAR-ES-SALAAM: Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile ametembelea Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na kuitaka bodi na menejimenti kuhakikisha inaharakisha ukamilifu wa mradi wa majengo na miundombinu ya kisasa ya Chuo cha Usafiri wa Anga(CATC).

Akipokea taarifa kuhusu hatua zilizofikiwa katika  utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa majengo ya CATC utakaogharimu takribani shilingi Bilioni 78 hadi kukamilika kwake.jijini Dar-es-salaam, Kihenzile  amesema Mradi huo unagharamiwa na Serikali kwa asilimia mia moja unategemea kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo.

SOMA: Waziri Mbarawa amshukuru Samia miradi uchukuzi

Advertisement

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TCAA Dkt. Hamis Mwinyimvua ametoa shukran kwa serikali hatua yake ya  kuubeba kwa uzito mradi huo  wa CATC kwa kuutengea fedha na kuhakikisha unatekelezwa kikamilifu.

Awali  akiwasilisha taarifa kwa Naibu Waziri, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Daniel Malanga alisema kwa sasa wapo katika mchakato wa kumpata mkandarasi mjenzi na pindi hatua hii ikikamilika ujenzi utaanza mara moja.

SOMA:https://www.tcaa.go.tz/

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Waziri Kihenzile amesisitiza hatua zote zizingatie muda ili kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati.

“Sina shaka na weledi wa TCAA katika utekelezaji wa majukumu mliyokasimiwa, wito wangu ni kuwa  mzingatie maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwakuwa ana malengo makubwa ya kuhakikisha sekta ya Anga inakua nchini” alisema Mhe. Kihenzile

Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania ni moja kati ya vyuo vinavyotoa kozi ya Usalama wa Usafiri wa Anga (ASTC) na ni moja kati ya vyuo tisa vyenye sifa hizo Afrika na 35 duniani.