TCB yajitosa tamasha la filamu, sanaa
DAR ES SALAAM: Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imeungana na wadau wengine wa sanaa katika kikao kazi cha uzinduzi wa Tamasha la Kimataifa la Maendeleo ya Filamu na Sanaa Tanzania linalotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Tamasha hilo ambalo litafanyika Desemba, mwaka huu linaratibiwa na taasisi ya FAGDI (Foundation Ambassadors Gender Development Initiatives) kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania.
Tamasha hili linawakutanisha wadau wa filamu na sanaa na wadau kutoka sekta mtambuka katika jukwaa moja kujadili mustakabali wa maendeleo ya sekta hiyo kitaifa na kimataifa. Kutokana na changamoto kadha wa kadha zinazoikabili tasnia, tamasha hili litakuwa sehemu sahihi ya kuwasilisha changamoto hizo, kupata ufumbuzi wake na kupanga mipango endelevu.
Akiiwakilisha TCB katika kikao hicho, Meneja Mkuu Kitengo cha Masoko wa taasisi hiyo ya fedha, Janeth Zoya, ameelezea umuhimu wa tamasha hilo nguvu yake katika jamii ya Tanzania.
SOMA: TCB kushirikiana na SMZ kukuza uchumi
“Benki ya TCB tunatambua nguvu ya sanaa katika kuleta mabadiliko ndani ya jamii. Sanaa ni zaidi ya burudani, ni chanzo cha kukuza uchumi, kuchochea umoja wa kitaifa na kutambulisha utamaduni wetu duniani. Tasnia ya filamu na sanaa ina uwezo mkubwa wa kutuvusha nje ya mipaka, kusimulia hadithi na urithi wetu, na kuonyesha ufahari wa tamaduni za Kitanzania duniani,” alisema.
Zoya alisisitiza mbele ya wadau hao kuwa aliendelea kusisitiza umuhimu wa tamasha hilo kwa kusema:
“Tamasha hili litatoa fursa muhimu ya kuwakutanisha pamoja wadau mbalimbali kujadili mikakati itakayokuza uchumi na maendeleo ya sekta hii.
“Hivyo, ni vizuri kutumia fursa hii kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta, zikiwemo zile zinazohusiana na uwezeshwaji, uelimishaji na upatikanaji wa masoko. Lakini la muhimu zaidi, tunapaswa kutambua fursa zilizopo mbele yetu – uwezekano wa kufanya ushirikiano kimataifa, matumizi ya majukwaa ya kidigitali ili kuifikia hadhara ya kimataifa na kutengeneza muundo endelevu utakaowezesha mafanikio ya muda mrefu.”
Udhamini wa Benki ya TCB katika uzinduzi huu unaimarisha dhamira yake ya kusaidia miradi mbalimbali inayochangia maendeleo ya utamaduni na uchumi nchini.
Benki ya TCB inakusudia kuchangia katika kukuza maendeleo ya sanaa bunifu na sekta hiyo kwa ujumla ambayo inalenga kuchangia uanzishwaji wa sekta mahiri ya sanaa na utamaduni