TCB yatoa mikopo ya Sh trilioni 1.1 kuwezesha wajasiriamali

DAR ES SALAAM: Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imetoa jumla ya mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.1 tangu kuanzishwa kwake huku ikizindua huduma ya LIPA POPOTE kwa lengo la kurahisisha ufanyaji wa biashara.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Biashara kwa wateja wadogo na wakati  wa TCB, Lilian Mtali wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo jijini Dar es Salaam, Jumatano huku akisitiza LIPA POPOTE imeanzishwa ili kuondoa vikwazo katika miamala na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuinua uchumi wa kidijiti.

Kwa mujibu wa Mtali, kupitia huduma hiyo, wafanyabiashara wa kati na wadogo wanaweza kupokea malipo bila makato yeyote kutoka kutoka mitandao yote ya simu na benki.

Advertisement

Naye Ofisa Mkuu wa Huduma za kidijitali na ubunifu benki hiyo, Jesse Jackson ameeleza kuwa takwimu zimeonesha kuwa asilimia 14 ya Watanzania hutumia huduma ya lipa namba na kuongeza kuwa ujio wa huduma ya LIPA POPOTE umelenga kuongeza uelewa ,matumizi ya malipo na kuchagiza ukuaji wa uchumi.

SOMA: TCB yajitosa tamasha la filamu, sanaa

Aidha huduma hiyo imetajwa kushughulikia hitaji la malipo ya kifedha linaloongezeka kwa kasi nchini miongoni mwa wajasiriamali wadogo na wakati ambao ni uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa kwani huchangia asilimia 30 ya pato la taifa.

Naye ofisa mtendaji mkuu wa TCB, Adam Mihayo amesema kuwa mabadiliko ya kidijiti yanachangia kwa kiasi kuamua namna uchumi unavyokwenda, jambo limeisukuma benki hiyo kuwa mstari wa mbele wa kutoa huduma za kibunifu ambazo zitachochea ujumuishi wa kifedha na uwezeshaji.