TCRA -CCC yatahadharisha matumizi ya mitandao kwa watoto

BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA CCC), wametahadharisha wazazi kuwa makini na watoto katika matumizi ya mitandao ili kuepuka changamoto za kuwasiliana na watu wasiofaa wakiwemo wahalifu wa mitandao.

Akizungumza katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara ‘Sabasaba 2023’ Mkuu wa Idara ya Elimu na Uhamasishaji kutoka TCRA – CCC Hilary Tesha amesema wazazi wanapaswa kuchukua tahadhari nne muhimu na kutoruhusu matumizi ya mitandao kwa watoto.

“Kwenye mitandao kuna wahalifu ambao wanatumia njia za ulaghai kuwashawishi watoto kutoa taarifa nyeti kuhusu wao wenyewe au wazazi wao.”Amesema

Advertisement

Pia, kuna wanyanyasaji wa mitandaoni ‘Cyber Bullies’ ambao mara nyingi huwa na malengo ya kuwanyanyasa watoto kisaikolojia na kuwasababishia hofu au msongo wa mawazo.

“Mafataki wa mtandaoni ‘Online Sexual Predators’ ambao lengo lao ni kuwarubuni watoto kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi.”Amesema

Amesema pia, kukumbana na maudhui yasiyofaa kama vile maudhui ya ngono na picha za utupu, matukio ya kihalifu na biashara haramu na habari potofu.

“Kupakua programu hatarishi au virusi vya kompyuta kupitia tovuti hatarishi, kubofya viunganishi hatarishi na pia kufungua viambatanisho vya barua pepe vyenye virusi vya kompyuta na hivyo kusababisha uharibifu wa taarifa na vifaa vya kielektroniki.”Amesema

Tesha, amesema pia changamoto nyingine ni watoto kuingia kwenye matumizi ya simu kupindukia kutokana na fursa zinazopatikana mitandaoni kama vile michezo ya kompyuta, mitandao ya kijamii, katuni na muziki huwavutia sana watoto ambao baada ya muda huwafanya kuwa watumwa wa mitandao.

“Changamoto hizi zinaweza kupelekea kushuka kwa maendeleo ya watoto kitaaluma na kupata athari nyingine za kisaikolojia kama vile kuwa na msongo wa mawazo.”Amesema.

Aidha, amewataka wazazi kuwalinda watoto kwa kuwahamasisha kutumia mitandao ili umsaidie kwenye masomo yake kitaaluma zaidi na si vinginevyo.

“Mzazi ajifunze mitandao kwa upana wake kutamsiadia kuelewa athari, lakini pia kumsaidia kuzungumza na watoto wako, kuweka mipaka ya mambo ambayo mtoto anaweza na ambayo hawezi kuyafanya mtandaoni.”Amesema

Amesema, ni muhimu kuweka masharti kwa mtoto ili ajue mipaka yake pindi awapo mtandaoni na sio kusubiri hadi kitu kibaya kitokee kwake.

5 comments

Comments are closed.