MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) imesitisha kwa siku 30 leseni ya huduma za maudhui mtandaoni za Mwananchi Communicaions Limited kutokana na kuchapisha maudhui yaliyokatazwa na yanapingana na sheria.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Jabiri Bakari imesema Oktoba 01, 2024 Mwananchi Communications Limited ilichapisha maudhui mjongeo na sauti kwenye mitandao yake ya kijamii, maudhui yaliyozuiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 16 ya maudhui Mtandaoni.
SOMA: Kanuni mpya TCRA kufaidisha watengeneza maudhui mtandaoni
Taarifa imesema katika utoaji huduma na kwa mujibu wa kanuni ya 16 ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020, Mwananchi Communications Limited anatakiwa kutotangaza au kuchapisha kwa Umma maudhui yaliyozuiwa ikiwa ni pamoja na maudhui yanayolanga kudhihaki au kuharibu taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“UMMA UNATARIFIWA KUWA, kufuatia kuchapishwa kwa maudhui yaliyokatazwa na yanayopingana na sheria, TCRA imesitisha kwa muda leseni za huduma za maudhui za mtandaoni(online media services ) za Mwananchi Communications Limited(The Citizen, Mwananchi Digital, Mwananchi na Mwanaspoti) kutoa huduma za maudhui mtandaoni nchini Tanzania kwa muda wa siku thelathini(30) tangu tarehe ya kutolewa kwa taarafa hii, wakati masuala mengine ya kiusimamizi yanafanyiwa kazi,” imesema taarifa.
Taarifa hiyo imesema maudhui hayo yameleta tafsiri hasi kwa Taifa, jambo ambalo linaathiri na kuharibu Umoja, amani na mshikamano wa kitaifa.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania iliyoanzishwa kwa sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano Tanzania namba 12 ya mwaka 2003 ina jukumu la kusimamia huduma za mawasiliano ya Kielektroniki na Posta hapa nchini.