TCU yaongeza muda udahili shahada ya kwanza

MOROGORO: TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetoa fursa nyingine ya kuongeza muda wa udahili wa shahada ya kwanza katika programu ambazo bado zina nafasi kwenye vyuo vikuu nchini kwa mwaka wa masomo 2025/2026.
TCU imeongeza muda huo wa udahili kwa kufungua awamu ya tatu na ya mwisho itakayoanza Oktoba 6, hadi kufikia Oktoba 10 mwaka huu.
Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Profesa Charles Kihampa ,amesema hayo Oktoba 3, 2025 akizungimza na waandishi wa habari mjini Morogoro.
Amesema tume imeongeza muda wa udahili kwa kufungua awamu ya tatu baada kupokea maombi ya kuongeza muda wa udahili kutoka Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO).
Profesa Kihampa amesema maombi mengine yaliyopokelewa na Tume ni kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu kwa ajili ya waombaji ambao hawa kufanikiwa kupata udahili katika awamu ya kwanza na ya pili kwa programu ambazo bado zina nafasi.
“Kufuatia maombi hayo na kuyapata , na baadaya kuyafanyia uchambuzi imeonekana ni busara sasa Tume imefungua dirisha lingine litakuwa ni dirisha la tatu na la mwisho na litatunguliwa jumatatu Oktoba 6 na litakamilika Oktoba 10, “ 2025 na nafasi zilizobaki ni chache na waombaji watumie muda huo,” amesema Profesa Kihamba.
Profesa Kihamba amesema ,kuwa udahili wa shahada ya mwaka wa kwanza kwa ajili ya mwaka wa masomo wa 2025 /26 ulianza Julai15 kwa awamu ya kwanza na ulikamilika Augosti 10 na baadaye kufunguliwa awamu pili Septemba 3, na kukamilika Septemba 21, mwaka huu.

Amesema baada ya kukamilika awamu ya pili ilikuwa ni jukumu la vyuo kuweza kuchakata majina ya waliomba na vinaendelea kuchakata na kupitisha katika mabaraza yao kwa maana ya Seneti na Bodi kwa ajili ya kutoa idhini kwa wale ambao wamekidhi na wale ambao hawakukidhi vigezo kuwapa taarifa sababu za kutokukidhi kwao.
Katibu Mtendaji wa Tume hiyo amesema kwa wale ambao wamepata udahili kwa awamu ya pili , matokeo ya udahili yatatangazwa na Vyuo vya Elimu ya Juu Oktoba 6, 2025.
“Awamu ya kwanza ilikamilika na tuliitangaza ,na awamu ya pili imetamilika na matokeo yake sasa kwa wale waliopata na waliokosa yatatangazwa na Vyuo husika vya elimu ya juu siku ya jumatatu Oktoba 6,2025,” amesema Profesa Kihamba.
“Kwa wale ambao wamepata chuo zaidi ya kimoja watapokea ujumbe mfupi kupitia simu na tunawapa namba ya siri ambayo wataweza kujidhibitisha kwenye chuo kimoja wapo hii ni pamoja na wale wa awamu ya kwanza walichangua chuo zaidi ya kimoja nao ni muda wao kuchagua kimoja wapo na kuthibitisha kuanzia Oktoba 6 hadi 19 Oktoba 2025, “amesisitza.



