BARAZA la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania, (TEC) wanafanya Kongamano Kubwa la Kitaifa litakalo jadili ni namna gani Watanzania wanaweza kushiriki katika mfumo wa uchumi shirikishi na jumuishi nchini.
Kongamano hilo litakalofanyika leo (Juni 17) katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) litakalofunguliwa rasmi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Chemba.
Akizungumza Jijini hapa, Katibu Mkuu TEC, Padre Charles Kitima amesema Kongamano hilo litashirikisha wasomi takribani 2,000 wakiwemo wahadhiri na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, wabunge ambao ni watunga sera na wasomi wabobevu wa uchumi mbalimbali nchini.
Katika kongamano hilo watoa mada mbalimbali watajikita katika kuelimisha faida za mifumo mbalimbali na watatoa fursa kwa wasomi kujadili na kuwaeleza watanzania ni mfumo gani unaweza kuwasaidia wakashiriki kwenye uchumi shirikishi kwa kutumia vipaji na karama walizopewa na Mwenyezi Mungu.
“Awali watanzania walifuata mfumo wa ujamaa baadaye ukaja mfumo wa soko huria lakini katika Kongamano hilo watajadili ni mfumo gani utawapa fursa ya kushiriki katika kutumia raslimali za nchi,” alisema.
Padre Kitima alisema, Makongamano hayo yaliyoanza kufanyika tangu mwaka 2016, yanalenga kuwafikia Watanzania wote nchini na lengo ni kuwaelimisha kuhusu faida za mfumo wa uchumi shirikishi ambao umekuwa chimbuko la maendeleo katika nchi mbalimbali duniani kwani jamii yote wanashiriki katika kumiliki raslimali za umma.
Kabla wasomi mbalimbali kutoka vyuo vikuu mbalimbali kikiwemo Mzumbe walifanya utafiti na kubaini kwamba mfumo wa uchumi Shirikishi umepata mafanikio makubwa katika nchi mbalimbali zikiwemo Ujerumani, Austria, Uswisi, nchi za Scandinavia pamoja na Kanada ambazo zina maendeleo makubwa.
Padre Kitime alisema Kongamano hilo litawapa nafasi wasomi kujadili namna gani Watanzania watashiriki katika uchumi na kutumia raslimali za umma kwa usawa na kusaidia kuziba pengo la walionacho na wasio nacho nchini.
Naye mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk Donath Olomi alisema Kongamano hilo pia litajadili ni namna gani kundi kubwa la vijana linaweza kushiriki katika uchumi Shirikishi au jumuishi kwa lengo la kujenga taifa imara na endelevu.
Mpango wa kufanya makongamano hayo ni endelevu na lengo ni kuwafikia Watanzania wote kupitia njia mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari hivyo baada ya hilo la Dodoma watakwenda kufanya lingine mkoani Arusha.
Mwisho