TEC yatangaza maombolezo, misa siku 9 mfululizo

BAADA ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis kufariki duniani Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetangaza siku tisa mfululuzo za maombolezo za kiongozi huyo wa kiroho.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padri Dk Charles Kitima alibainisha hayo jana mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari makoa makuu ya baraza hilo Kurasini.
Dk Kitima alisema kutakuwa na misa kila siku katika siku hizo za maombolezo.
“Tunaamini mtu ambaye yupo njiani hajafika bado kwa Baba atakuwa na mapungufu ya kutokuwa kabisa kama anavyotaka Baba wa mbinguni tunaimani hiyo sala ina nguvu ya kutosha,” alisema.
Alisema taratibu za mazishi zinaendelea kuratibiwa na kubainisha kuwa bado tarehe rasmi ya mazishi ya Papa Francis haijafahamika na kuwa kwa sasa taratibu za maamuzi katika ofisi ya Papa zimesimama hadi pale atakapochaguliwa mwingine.
“Ni kipindi cha mpito lakini uzuri kunakuwa na anayeongoza shughuli za ndani za kawaida za kiutendaji lakini za kimaamuzi na sera zinasimama mpaka Papa mwingine apatikane,” alisema.
Alisema hakutakuwa na shughuli ya kitaifa kwa ajili ya mazishi ya Papa na kuwataka ambao wanataka kutoa salamu za rambirambi na kusaini kitabu cha maombolezo kufika katika Ofisi ya Ubalozi wa Vatican Tanzania.
Dk Kitima alisema Papa mpya atapatikana ndani ya muda wa siku 15 hadi 20 na makardinali wenye umri wa chini ya miaka 81 kutoka kote duniani watakutana na kumchagua Papa mpya.
Alisema katika uchuguzi wa Papa mpya utakaofanyika baadaye Tanzania itawakilishwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa.
“Sisi tuna bahati tumepata Kadinali mpya mwaka juzi Protase Rugambwa wa Jimbo Kuu la Tabora watanzania tuna mshiriki ataenda kupiga kura ama kupigiwa kura,” alisema.
Kuhusu nafasi ya Afrika kutoa Papa ajae baada kifo cha Papa Francis, Padri Kitima alisema jambo hilo lipo mikononi mwa Mungu ndio anafayefahamu ni kiongozi gani atafuata na atatokea wapi kutokana na uhitaji wa Kanisa na dunia.
“Mchakato wa viongozi wa kiroho tuuwache katika mtindo ambao tunasema Mungu anauongoza hawaangalii kuwa kule kuna makadinali wengi wapigiane kampeni hapana hicho ni kitu ambacho hakiruhusiwi kabisa,” alisema.
Akizungumzia kuhusu maisha ya Papa Francis, Padri Kitima alisema alikuwa ni kiongozi mwenye huruma ambaye alipenda kuona watu wakitoka katika dimbwi la umasiki kwa kuwezeshwa kupitia njia mbalimbali ili wairudi katika umasikini.
“Alipochaguliwa alitoa mfano, alisema jamani kama kuna mtu ana jozi nne za viatu jozi moja si ya kwako unapaswa kuwa na jozi tatu hiyo jozi moja mpe mwingine ambaye hana ukienda sasa hivi pale Vatican kuna mahali wanatoa mlo mchana na jioni kila siku kwa sababu kuna watu wanaishi pale Roma mjini lakini hawana chakula,” alisema.
buy viagra online