KUONGEZEKA kwa matumizi ya mitandao ya kijamii kumeleta aina mpya ya ukatili dhidi ya wanawake hasa wakati huu kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam juzi na Mkurugenzi wa Women in Management Africa (WIMA) Dk. Naiken Moshi kwenye warsha ya namna ya kukabiliana na changamoto za ukatili wa kijinsia wa wanawake kwenye siasa za Tanzania.
Warsha hiyo iliandaliwa na taasisi binafsi ya Imara Leadership Initiative Tanzania chini ya msaada wa mfuko wa Kodi Annan, Ushirikiano wa Ulaya kwa Demokrasia (EPD), Taasisi yay a Demokrasia ya Westmister (WFD) na kituo cha Oslo katika mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya.
Imara inajihusisha na masuala ya Wanawake na Vijana kwenye Demokrasia (WYDE).
“Mimi binafsi nilijitoa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuona nashambuliwa bila sababu,” alisema.
Alisema jamii haina budi kuyaoa kipaumbele masuala ya unyanyasaji wa kijinsi ili kuwa na jamii yenye ustawi kwa wanawake.
“Kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mikakati ya namna ya kulishughulikia hili ili kumaliza tatizo la wanawake kushambuliwa kwenye mitandao,” alisema.
“Nimefurahi kualikwa hapa, nimefurahi zaidi kuona washiriki wote wa warsha hii ni vijana, ndio muhimu kuwa na vijana kwenye uongozi hivyo ni vema kuanza kujifunza kuanzia sasa maana sisi ndio tunamaliza hivyo mtabaki nyie,” alisema Dk. Naike.
Alisema midahalo na warsha kma hizo ni muhimu kwa wanawake kwa kuwa nchi inaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika nchi nzima Novemba 27 mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.
“Lengo ni kuwahamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbali mbali za uongozi na kuongeza ujuzi katika kukuza demokrasia,” alisema.
Akizungumzia warsha hiyo mjumbe wa WYDE Tanzania Petrider Paul alisema kutokana na miradi ya taasisi hiyo wanawake wanapata fursa ya kujifunza demokrasia.
“Lakini pia tunaelimisha jamii kuhusu njia za kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa wanawake viongozi nchini “, alisema.