Utekelezaji hafifu wa Sera watajwa chanzo cha ukatili kijinsia

DAR ES SALAAM : Kukithiri kwa ukatili na ndoa za utotoni ni hatua inayotokana na sera na sheria kutofanyiwa kazi katika jamii, wazazi kutokuwa na uelewa mzuri, mila kandamizi na ukosefu wa vifaa tiba, hali inayosababisha watoto wengi wa kike kukosa haki zao za msingi kama vile elimu.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Uwezeshaji Wasichana wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Lilian kimath, wakati akizungumza na wanahabari katika semina ya kuwajengea uwezo juu ya masuala ya ndoa za utotoni, iliyofanyika Makao Makuu ya shirika hilo Mbezi jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Irene Ernest akizungumza wakati wa semina hiyo ameeleza namna ambavyo shirika linashirikiana na taasisi mbalimbali, kutoa elimu kwa jamii katika ngazi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa mtoto wa kike anakuwa salama.

Naye, Mratibu wa Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMIN) Waikili Irene Nambuo, akizungumza na waandishi wa habari amesema ili kutokomeza ndoa za utotoni ipo haja ya kuangalia upya sheria kandamizi na kuzifanyia kazi, ili kuweka usawa.
Hadi sasa shirika hilo limefanikiwa kufikia wasichana 2000 na kuwapa elimu, kuwasaidia katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja nab kujenga madawati ya kijinsia, kusapoti juhudi za Serikali ili kuondoa dhana hiyo katika jamii.



