Teknolojia ni suluhisho la kuboresha ufundishaji, upatikanaji wa elimu nchini

ARUSHA: TUNAISHI katika dunia ambayo kwa kiasi kikubwa imetawaliwa na matumizi ya teknolojia za kidigitali. Athari za teknolojia zinaweza kuonekana katika upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwenye maisha yetu ya kila siku.

Teknolojia hususani ya habari na mawasiliano imebadili mfumo wa ufanyikaji wa shughuli nyingi za sekta za umma na binafsi ikiwemo elimu ambayo imekuwa ikinufaika kwa kiasi kikubwa kwa ubunifu na maboresho ya namna za ufundishaji wa walimu na kujisomea kwa wanafunzi nchini.

Kila mwaka Asasi za Kiraia (AZAKI) nchini hufanya kongamano lijulikanalo kama ‘WIKI YA AZAKI’ ambalo huikutanisha serikali pamoja na taasisi mbalimbali za kiraia kutoka sekta za umma na binafsi kujadili masuala tofauti kwa manufaa ya maendeleo ya Watanzania.

Kwa mwaka 2023, Wiki ya AZAKI ilifanyika kuanzia Oktoba 23 mpaka Oktoba 27 jijini Arusha ikiwa na kauli mbiu isemayo ‘Teknologia na Jamii: Tulipotoka, tulipo sasa na tunapoelekea, kuangazia fursa na changamoto zinazotokana na ulimwengu wa teknolojia unaoendelea’.

Vodacom Tanzania Foundation ambayo ni sehemu ya kampuni ya Vodacom Tanzania ikiwa imejikita katika shughuli za kurudisha kwa jamii ikiangazia zaidi sekta za afya, elimu, uwezeshaji wa uchumi jumuishi, na mazingira, ilikuwa ni mojawapo ya washiriki kwa mwaka huu.

Katika maadhimisho hayo, taasisi hii ilikuwa ni miongoni wa washirika muhimu, ikiwasilisha mchango wa matumizi ya teknolojia ya simu za mkononi na mchango wake katika sekta ya elimu, kwa kuanzisha suluhisho za kibunifu za kielimu.

Kwa mfano, jukwaa lake la kujifunzia mtandaoni, e-Fahamu, na umuhimu wa elimu kwa kidigitali katika kupunguza pengo huduma ya elimu nchini.

E-Fahamu ilianzishwa na taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation mwaka 2017 kwa lengo la kusaidia wanaojifunza upatikanaji wa masomo kwa njia ya kidigitali. Tovuti hii hukusanya maudhui ya ndani na kimataifa, yakiwa yameandaliwa mahususi kwa ajili ya wanafunzi na walimu katika mfumo wa video na PDF. Pia, inayo maudhui kutoka Taasisi ya Elimu ya Tanzania, maktaba ya kidigitali iliyosheheni rasilimali kwa ajili ya shule za sekondari kama vile vitabu mbalimbali.

Tovuti ya e-Fahamu inapatikana bila ya matumizi ya data kwa wateja wa mtandao wa Vodacom, ambapo wanaweza kuitumia kupitia simu zao za mkononi au kompyuta.

Malengo ya kuanzisha tovuti kama hii ni kuhakikisha watu wanaopenda kujifunza nchini wanapata nyenzo za kujifunzia kwa urahisi, pamoja na kuwezesha upatikanaji wa elimu kwa wale ambao hawakupata fursa ya kusoma elimu rasmi.

Taasisi inashirikiana na wadau kutoka sekta za umma na binafsi kueneza tovuti ya e-Fahamu kwenye shule za sekondari. Imeshirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na taasisi ya African Child Projects, tangu mwaka 2019 chini ya mwavuli wa programu ya Uunganishwaji wa Shule ambapo ushirikiano huu hukusanya kwa pamoja rasilimali kama vile nyenzo za kidigitali, mafunzo kwa walimu na uunganishwaji wa intaneti kuziwezesha shule kupata mafunzo na elimu ya kidigitali.

Mpaka sasa, taasisi hii kupitia ushirikiano huu, imewafikia wanafunzi zaidi ya 600,000, shule za sekondari 900, na walimu zaidi ya 15,000.

Akizungumza katika Wiki ya AZAKI 2023 namna ambavyo serikali inavyoshughulikia sera na mifumo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Mhandisi Samson Mwela amesema kuwa, “serikali imekuwa ikifanyia kazi sera na mifumo ambayo inaunga mkono ubunifu nchini.

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imeweka kipaumbele ubunifu, kupitia Dar Teknohama Business Incubator (DTBi). Vilevile, kumepelekea kuibuka kwa programu nyingi kama vile ya Vodacom Digital Accelerator. Kuhakikisha teknolojia inaleta maendeleo, lazima tuzitazame tena sera ambazo zinakwamisha ubunifu au zilizopitwa na wakati.”

Habari Zifananazo

Back to top button