TEMDO yaita wadau kilimo, afya, viwanda kununua vifaa vya kisasa

WAKULIMA na wenye viwanda nchini wameombwa kutembelea Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) kujionea mashine zinazotatua changamoto ya sekta ya kilimo na viwanda nchini ikiwemo kujikwamua kiuchumi kwa kuongeza thamani ya mazao.

Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Temdo, Profesa Frederick Kahimba wakati wa ziara ya makatibu wakuu wa kisekta waliofika kujionea zana za kilimo na za afya zinazotengenezwa katika taasisi hiyo.

Profesa Kahimba amesema taasisi hiyo imejikita kutatua changamoto za wakulima na wenye viwanda kwa kubuni na kutengeneza mashine zinazoendana na mahitaji ya wakulima kama vile za kubangua korosho, kupukuchua mahindi, viungo vya chai, mashine za mafuta ya kula na vitanda katika sekta ya afya.

Pia, amesema taasisi hiyo imejikita kutatua changamoto wanazokumbana nazo wakulima shambani kwa kutengeneza mashine ndogo zenye ubora ambazo zitawasaidia wakulima kutatua changamoto zao shambani na kupeleka mazao yao sokoni yakiwa na ubora zaidi.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Temdo, Profesa Lazaro Busagala amesema taasisi hiyo inazalisha bidhaa zaidi ya 16, hivyo aliwasihi wadau kutembelea taasisi hiyo na kujionea aina za vifaatiba na mashine zinazoweza kutatua changamoto za wakulima na kuwezesha kuongeza thamani ya mazao kutokana na uhitaji wa soko husika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button